"Nadhani niko kwenye mahaba" Carol Muthoni adai baada ya Madini Classic kudokeza mahusiano naye

Muhtasari

•Madini Classic alipakia picha akiwa amemkumbatia mpenzi huyo wa zamani wa mchekeshaji Mulamwah na kuiambatanisha na ujumbe ambao ulidokeza mahusiano kati yao.

•Jumapili Muthoni aliendelea kuwachanganya wanamitandao huku akipakia ujumbe ambao ulidokeza kuwa amejitosa kwenye mahusiano mapya.

Image: INSTAGRAM// MADINI CLASSIC

Siku za hivi majuzi mwigizaji Carol Muthoni na mwanamuziki Madini Classic wamekuwa mada ya mazungumzo kwenye mitandao baada yao kuonekana pamoja katika hali tatanishi.

Mnamo Jumamosi Madini Classic alipakia picha akiwa amemkumbatia mpenzi huyo wa zamani wa mchekeshaji Mulamwah na kuiambatanisha na ujumbe ambao ulidokeza mahusiano kati yao.

"Niite Mr. Polygamous. Mke wa pili," Madini aliandika chini ya picha yake na Muthoni.

Chapisho hilo limeibua hisia tofauti miongoni mwa wanamitandao huku wengi wakihoji iwapo ni kweli wawili hao wanachumbiana ama wanatafuta kiki tu.

Mnamo Jumapili Muthoni aliendelea kuwachanganya wanamitandao huku akipakia ujumbe ambao ulidokeza kuwa amejitosa kwenye mahusiano mapya.

"Nadhani niko kwenye mahaba," Muthoni aliandika chini ya video yake ambayo alipakia Instagram.

Wanamitandao walijumuika chini ya chapisho la mzazi huyo mwenza wa Mulamwah wakitaka kufafanuliwa zaidi kuhusiana na ujumbe wake.

Madini ni mmoja wa walioacha ujumbe chini ya chapisho la Muthoni.

"❤️❤️❤️❤️❤️❤️ Superwoman🌹" Aliandika.

Mwanamuziki huyo pia alichapisha video hiyo ya Muthoni kwenye ukurasa wake.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa wawili hao wanatafuta kiki kuona kuwa Muthoni ni mwigizaji ambaye amewahi kuhusika katika nyimbo na vipindi kadhaa.

Katika mahojiano ya hivi majuzi Muthoni amekuwa akidai kuwa hayuko tayari kujitosa kwenye mahusiano mengine kwa sasa ila hajatupilia uwezekano wa kupenda tena  baadae.