"Nahitaji maombi yenu!" Jimal aweka wazi baada ya aliyekuwa mkewe, Amira kuenda Tanzania

“Kwa sasa yuko Tz. Watu wa Mungu nahitaji maombi yenu,” alisema

Muhtasari

•Alipanda ndege kwenye Uwanja wa Ndege  wa Jomo Kenyatta  siku ya Jumapili jioni hadi jijini Dar es Salaam.

•Mapema siku hiyo, alidai kuwa mtu asiyemtaja alienda mahali ambako hakufichua 'kuongeza nguvu'. 

Amira na aliyekuwa mumewe, Jamal Rohosafi
Image: INSTAGRAM

Inaonekana kama nafsi ya mfanyibiashara mashuhuri na ambaye ni Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu jijini Nairobi, Jimal Marlow Rohosafi  bado ameshikamana na mke wake wa zamani Amira.

Amira, ambaye ana watoto wawili na Jimal, kwa sasa yuko katika nchi jirani ya Tanzania kwa ziara ambayo hajabainisha.

Alipanda ndege kwenye Uwanja wa Ndege  wa Jomo Kenyatta  siku ya Jumapili jioni hadi jijini Dar es Salaam. Alichapisha picha zinazomuonyesha akitembelea maduka ya Milimani City Mall na duka la Pips by Rae.

Huku mfanyibiashara huyo akiwa Tanzania, mumewe wa zamani, Jimal yuko nchini Kenya akiomba kuombewa. Jumatatu alasiri, Jimal alisema mwanamke ambaye hakumtaja yuko Tanzania na hivyo akawaomba watu wamuombee.

“Kwa sasa yuko Tz. Watu wa Mungu nahitaji maombi yenu,” alisema kupitia Instagram.

Mapema siku hiyo, alidai kuwa mtu asiyemtaja alienda mahali ambako hakufichua 'kuongeza nguvu'. Kufuatia hilo, baba huyo wa watoto wawili alimtaka mtu huyo kumrudia Mungu na kutia bidii ili kufanikiwa.

"Akili ya mtu fulani huwa haitulii kamwe. Hata uende wapi kuongeza nguvo hiyo tushajua. Ushauri wangu 'Rudi kwa Mungu, fanya kazi kwa bidii na usonge mbele na maisha yako," aliandika kwenye Instastori.

Julai mwaka jana, Jimal alimuomba radhi mama huyo wa watoto wake wawili kwa drama nyingi alizosababisha kwenye ndoa yao mwaka 2021.

Katika ombi lake la msamaha Jimal alikiri kuwa alimkosea sana mkewe kwa kutekeleza wajibu wake wa kumlinda.

Alimuomba mkewe apokee ombi lake la msamaha huku akimkumbusha jinsi ambavyo wamepitia mengi pamoja.

"Ilikuwa mbaya kabisa. Huenda nilionekana kama mtu asiye na wasiwasi lakini sikuwa na la kufanya. Nilijua haikuwa sawa, nilijua unaumia lakini sikuweza kujikusanya!Amira nafanya hivi kwa sababu ukosefu wa heshima pia ulikuwa mkubwa. Naomba radhi kwa kukosa heshima," Aliandika.

Mwenyekiti huyo wa muungano wa wamiliki matatu pia alifichua kwamba hajakuwa sawa tangu alipokosana na mke huyo wake.

Alidokeza kuwa yupo tayari kupiga hatua zozote ili kufufua ndoa yao iliyokufa miezi kadhaa iliyopita.

Katika jibu lake, Amira alisema hawezi kuuelewa msamaha wa mzazi mwenzake kwani ulifufua kumbukumbu ya siku mbaya za nyuma.

"Ombi hilo la msamaha limenirudisha katika sehemu moja ya giza ambayo nimewahi kuwa katika maisha yangu kwa sababu nimetafakari juu ya mengi yaliyotokea hadharani na nyuma ya milango iliyofungwa na imezua hisia nyingi," alijibu.

Mama huyo wa watoto wawili aliomba neema ya Mungu anapoendelea kutafakari suala hilo na kueleza kuwa kwa sasa amezidiwa na hisia.

"Vidonda vingine haviponi, lazima ujifunze jinsi ya kuishi navyo," Aliandika.