"Ndio nilitoroka!" Size 8 afichua sababu za kumuacha mumewe DJ Mo

Mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa alikuwa amegura ndoa yake baada ya DJ Mo kumkosea vibaya.

Muhtasari

•Size 8 ambaye kwa jina halisi ni Linet Munyali alithibitisha kwamba alikuwa amemuacha mumewe DJ Mo.

•Mwimbaji huyo alifichua kuwa watumishi wa Mungu waliwasaidia kupatana na kusuluhisha mzozo wao.

Image: INSTAGRAM// SIZE 8

Wanandoa mashuhuri DJ Mo na Size 8 hatimaye wamejitokeza kueleza hali halisi ya ndoa yao ya miaka mingi ambayo ilidaiwa kusambaratika.

Katika video waliyopakia kwenye YouTube, Size 8 ambaye kwa jina halisi ni Linet Munyali alithibitisha kwamba alikuwa amemuacha mumewe.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili aliweka wazi kuwa alikuwa amegura ndoa yake  baada ya mumewe  DJ Mo kumkosea vibaya.

"Ndio nilitoroka. Nilikuwa nimemkasirikia sana DJ Mo. Alinikosea. Nilihitaji tu nafasi yangu niweze kupumua na kuongea na Mungu kwa kuwa naamini nikiwa na hasira na tuko kwa nyumba moja tutaongeleshana vibaya na kufanyiana vibaya," Size 8 alisema huku akiwa amesimama sako kwa bako na mumewe.

Alidokeza kuwa kosa ambalo DJ Mo alimfanyia hadi kufanya atoroke ni kubwa, jambo ambalo mcheza santuri huyo alikiri.

"Ndio nilikosea, na nilisema pole," Mo alisema.

Size 8 alibainisha kuwa tatizo lililotikisa ndoa yao ya takriban mwongo mmoja ni la kawaida katika ndoa zote.

Alifichua kuwa watumishi wa Mungu na watu wengine wa karibu waliwasaidia kupatana na kusuluhisha mzozo wao.

"Tulifikia hitimisho na ufahamu wa kibiblia na sasa tumepatanishwa tena kwenye ndoa kwa sababu ya neema na rehema za Mungu," Alisema.

Aidha alifichua kuwa kipindi alichokuwa amekimbia ndoa yake na kuwabeba watoto wao Ladasha Wambui na Samue Muraya Jr, wawili hao walitamani sana kurudi nyumbani na hata kumuuliza ingefanyika lini. 

Wikendi ripoti nyingi zilisambaa mitandaoni zikidai kuwa mkewe Mo, Size 8 aligura ndoa yao pamoja na watoto wao na kuhamia kwingine.

Habari zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilisema mwimbaji huyo alidaiwa kubeba vitu vyake na kwenda kuishi kwingine bila mumewe DJ Mo kutokana na migogoro ya kinyumbani.

Iliripotiwa kuwa juhudi za marafiki na familia kuwapatanisha wawili hao hazikuzaa matunda kwani Size 8 alikuwa amemkasirikia sana mumewe.

Vyanzo vya habari vilisema mwimbaji huyo aliwaomba marafiki na wanafamilia waliojaribu kuwapatanisha kumpa muda wa kufikiria kuhusu ndoa yao.

Katika video waliyochapisha, Mo na Size waliweka wazi kuwa hakuna yeyote kati yao ambaye alichukua hatua ya kufahamisha vyombo vya habari kuhusu kutengana kwao.

Walisema siku tatu tayari zilikuwa zimepita baada ya Size 8 kuondoka wakati habari hizo zilipofichuka huku wakishangaa jinsi ambavyo ziliweza kupenyeza hadi kuwafikia waandishi wa habari.