Niliridhika na kidogo alichokuwa akinipa!- Babake Diamond amshauri baada ya kutapeliwa Sh240m

Mzee Abdul aliweka wazi kuwa hakutarajia mengi kutoka kwa mwanawe kwani pia naye anahitaji kujivinjari.

Muhtasari

•Mzee Abdul amesema hajisikii vibaya kusikia kwamba mwanawe aliwekeza mamilioni  katika juhudi za kununua ndege bila kumpa hata senti.

•Mzee Abdul alimshauri staa huyo wa bongo dhidi ya kutoa matamko kuhusu kitu kabla ya kuwa nacho mikononi mwake.

Diamond Platnumz, Mzee Abdul Juma Isack
Image: HISANI

Mzee Abdul Juma Isack, mzee anayeaminika kuwa baba mzazi wa Diamond Platnumz ameweka wazi kuwa hajisikii vibaya kusikia kwamba mwimbaji huyo wa bongo aliwekeza mamilioni ya pesa katika juhudi za kununua ndege binafsi bila kumpa hata senti.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Mbengo TV, mzee huyo aliweka wazi kuwa hakutarajia mengi kutoka kwa mwanawe kwani pia naye anahitaji kujivinjari.

Babake Diamond pia alikiri kuwa bosi huyo wa WCB alikuwa akimpa kitu kidogo katika siku za nyuma, ambacho aliridhika nacho.

“Vidogo vidogo alivyokuwa ananipa mwanzo vilikuwa vinanitosha. Chochote unachopata inabidi uridhike. Anajitahidi, anajiweka vizuri, inabidi anataka kuenjoy. Bado anataka kuenjoy yule ile ajue kazi yake inampa faida gani, ina umuhimu gani,” Mzee Abdul alisema.

Alisema hayo alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu ufichuzi wa hivi majuzi wa Diamond kwamba alitapeliwa Tsh 4b (Ksh240m) katika shughuli ya ununuzi wa ndege binafsi iliyofeli.

Mzee Abdul alibainisha kuwa huenda mwanawe alifanya makosa katika mchakato wa ununuzi wa ndege na kusababisha hasara kubwa ya fedha zake.

"Kama kweli alienda hasara, katika muda mwafaka, hiki kitu anaweza akakipata," Mzee Abdul alisema.

Alichukua fursa hiyo kumshauri staa huyo wa bongo dhidi ya kutoa matamko kuhusu kitu kabla ya kuwa nacho mikononi mwake.

Aidha, Mzee Abdul pia alimshauri mwanawe kufuata utaratibu sahihi katika ununuzi akimhakikishia kuwa hatimaye atafanikiwa kununua ndege hiyo.

“Ni bahati mbaya. Kuna watu wengine wajanja janja kapata riziki hapo katikati. Basi afanye kazi tena kwa bidii., ajaribu tena kuweka ili akipata ingine kamaa kupata, mwenyezi Mungu hawezi kumtupa. Kwa kuwa ashapata funzo, aende kwa mahitaji ya mahitaji,” alisema.

Mwezi uliopita, bosi wa WCB Diamond Platnumz alifichua kwamba alitapeliwa kitita cha Ksh 240,591, 200 milioni alipokuwa akinunua ndege yake binafsi.

Katika juhudi za kuwafafanulia mashabiki wake kwa nini anaendelea kusafiri kutumia ndege za kibinafsi za kukodi badala ya ndege zake, kama alivyotangaza hapo awali, alifichua hayo.

Kulingana na Diamond, alitapeliwa na ajenti aliyekuwa akimsaidia kununua ndege ya kibinafsi.

"Nilikuwa nimeleta ndege kubwa sana, lakini walinilaghai takriban Tsh bilioni 4," aliiambia Wasafi Media.

Aliendelea kusema kuwa amemshtaki tapeli huyo na kwamba mamlaka ya Tanzania inafuatilia suala hilo.

"Serikali inajua, ukiiba kiasi hicho cha pesa utarukwa na akili."

Diamond aliongeza kuwa ameanza kulipwa kwa awamu.

"Wameanza kulipa. Nilitarajia ndege ingetua hapa Agosti mwaka jana lakini hadi mwisho wa mwaka ilikuwa haijafika. Walinidharau kwa sababu walinifanya nionekane kama nimetangaza habari za uongo." alisema.