"Nina watu wanaoniombea" Otile Brown ajawa bashasha baada ya kurudishiwa laptop zake zilizoibiwa

Wanaume wawili walionekana wakirejesha tarakilishi hizo mbili.

Muhtasari

•Otile Brown alifichua habari hizo  njema kwenye Instagram ambapo alipakia video ya wanaume wawili wakirejesha tarakilishi hizo mbili.

•Brown alikuwa ametoa ombi kwa mtu aliyeiba tarakilishi hizo katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kuzirejesha.

Image: INSTAGRAM// OTILE BROWN

Siku ya Jumatano asubuhi, mwanamuziki wa Kenya Otile Brown alifanikiwa kuzipata tarakilishi zake mbili zilizoibiwa nchini Tanzania.

Otile Brown alifichua habari hizo  njema kwenye Instagram ambapo alipakia video ya wanaume wawili wakirejesha tarakilishi hizo mbili.

"Nina watu wanaoniombea kutoka dini tofauti," alisema baada ya kufichua kwamba amefanikiwa kuzipata mashine hizo zilizokuwa zimeibiwa.

Katika video hiyo, wanaume wawili waliovalia vizuri wanaonekana wakigonga mlango wa msanii huyo muda usiojulikana asubuhi.

Otile ambaye anaonekana kuamka muda mfupi tu kabla ya mlango kubishwa anaonekana akiwakaribisha wawili hao na kupokea tena laptop zake.

"Mmezipataje?" anasikika akiwauliza.

"Ni hadithi refu kaka," mmoja wao alijibu.

Mwimbaji huyo mahiri mwenye umri wa miaka 30 kisha anaendelea kukagua mashine zile na anaonekana kuridhishwa na hali aliyozipata.

Siku ya Jumanne, Brown alikuwa ametoa ombi kwa mtu aliyeiba tarakilishi hizo katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kuzirejesha.

Akizungumza kwenye video ambayo alichapisha kwenye Instastories zake, Brown alisema yuko tayari kumlipa yeyote aliyekuwa akishikilia kompyuta hizo zale za mkononi iwapo angechukua hatua ya kuzirejesha.

Alifichua kuwa mashine hizo zina vitu vyake muhimu sana ambavyo hataki kupoteza.

"Atakayepata laptop zangu mimi nitapeana hela. Mimi ni straight, hata sio lazima tuende kwa polisi," alisema.

Aliongeza, "Huenda saa hii unatafuta soko ya kuuza, unatafuta mteja. Content zilizo humo ndani ni muhimu sana. Mimi naweza nikakupa hela ukanirejeshea laptop zangu. Utakuwa umenifanyia favour kubwa sana,"

Mwanamuziki huyo alifichua kuwa hajapata utulivu na hakuwa ameweza kupata usingizi kufikia wakati alipokuwa akitengeneza video hiyo.

Alitoa nambari ya WhatsApp +25428248738 ili yeyote aliye na vitu vyake vilivyoibiwa awasiliane naye kwa mipango ya kurejesha.