Sarah Kabu adai ombi la msamaha kutoka kwa binti mkubwa wa mumewe Simon Kabu

Muhtasari

•Sarah alisema hakufurahishwa na tukio la mumewe, binti yake na watoto wao kuenda likizo ya siku kumi bila yeye kuwepo.

•Mfanyibiashara huyo alisema kuna takriban asilimia 10 ya masuala ambayo bado hayajatatuliwa katika familia yake.

Simon Kabu na mkewe Sarah Kabu
Simon Kabu na mkewe Sarah Kabu
Image: HISANI

Mkurugenzi Mtendaji wa Bonfire Adventures Sarah Kabu amefichua kuwa hali ya maelewano kamili bado haijarejea kwa familia yake.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Sarah alieleza kuwa bado anasubiri ombi la msamaha kutoka kwa mtoto wa kwanza Simon Kabu.

Mfanyibiashara huyo alisema hakufurahishwa na tukio la mumewe, binti yake na watoto wao kuenda likizo ya siku kumi bila yeye kuwepo.

"Kweli ni binti ya Simon lakini hatuna uhusiano. Lakini yeye ni mgeni kabisa. Yeye kuvua watoto wangu nguo ni jambo la kushtua. Watu wanaweza kuhukumu wengine lakini ata kama mimi ni mjasiri, ikifika kwa watoto wangu, mimi ni mdhaifu," Sarah Kabu alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alisema kuna takriban asilimia 10 ya masuala ambayo bado hayajatatuliwa katika familia yake.

Sarah hata hivyo aliweka wazi kuwa hana shida na mumewe. Alisisitiza kuwa anachotaka ni binti wa wake mwenye umri wa miaka 25 achukue hatua ya kuomba msamaha.

"Bado nasubiri ombi la msamaha. Bado hatujakaa chini na kutatua mambo yote. Naweza kusema 90% tuko sawa," Alisema.

MfanyIbiashara huyo alieleza kuwa hatua yake kulalamika hadharani mapema mwaka huu ilichangiwa na kiwewe alichopata baada ya watoto wake kuchukuliwa. 

"Nilikuwa navuma kwa sababu nilikuwa nalinda watoto wangu. Nahisi watoto ni wa thamani. Hicho ni kipindi kigumu zaidi kuwahi kupitia katika maisha yangu ya uzazi. Sikuwahi kufikiria eti mtu angekuja achukue watoto wangu bila ruhusa," Alisema.

Alifichua kuwa ilipita siku kumi bila yeye kuwaona watoto wake na ndiposa akachukua hatua alizochokua za kulalamika mitandaoni.

Sarah hata hivyo amesema kuwa anatazamia kusuluhisha shida zilizopo katika familia yake bila kuhusisha wanamitandao.