Sarah Michelloti arejea Tanzania, yadaiwa amerudi kudai mali yake kutoka kwa Harmonize

Mwanamitindo huyo alimtema Harmonize mwaka wa 2020 baada ya kuchumbiana kwa miaka minne.

Muhtasari

•Sarah aliwasili Tanzania siku kadhaa zilizopita na amekuwa akijivinjari katika kisiwa cha Zanzibar kilicho mashariki mwa Tanzania.

•Mwanamitindo huyo amekuwa akitumia ziara yake ya Tanzania kurudisha kumbukumbu za kipindi ambacho aliishi pale na pia kukutana na baadhi ya marafiki wake ambao aliwapata wakati huo.

Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake Sarah Michelloti
Image: HISANI

Bi Sarah Michelotti, mpenzi wa zamani wa staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize kwa sasa yuko nchini Tanzania.

Sarah aliwasili Tanzania siku kadhaa zilizopita na amekuwa akijivinjari katika kisiwa cha Zanzibar kilicho mashariki mwa Tanzania.

Katika kipindi cha wiki moja ambacho kimepita mwanamitindo huyo kutoka Italia amekuwa akipakia picha zinazomuonyesha akifurahia muda wake katika kisiwa hicho  na kufichua kuwa yuko katika kijiji cha Kiwengwa.

"Najihisi nyumbani... Zanzibari," Sarah aliandika chini ya chapisho la hivi majuzi.

Mwanamitindo huyo amekuwa akitumia ziara yake ya Tanzania kurudisha kumbukumbu za kipindi ambacho aliishi pale na pia kukutana na baadhi ya marafiki wake ambao aliwapata wakati huo.

Hata hivyo kumeibuka tetesi kuwa ameandamana na kundi kubwa la wanasheria na anakusudia kuvichukua vyote alivyompa Harmonize. Imedaiwa baadhi ya mali ambayo bosi huyo wa Konde Music Worldwide anamiliki ikiwemo lebo, nyumba na magari kadhaa ni ya mpenzi huyo wake wa zamani.

Sarah alimtema Harmonize mwaka wa 2020 baada ya kuwa kwenye mahusiano naye kwa takriban miaka minne.Mwaka jana Harmonize alitunga wimbo 'sorry' kwa ajili ya kumuomba msamaha mpenzi huyo wake wa zamani.

Mwimbaji huyo alisema ndoa yao ilianza kusambaratika wakati mpenziwe alikuwa amesafiri kuenda kwao na baada ya kuwa pweke kwa muda akapata majaribu ya kutembea na mwanadada aliyemzalia mtoto

"Mimi nilikuwa Tanzania na kama unavyojua umbali wa mapenzi unapokuwa nikaishia kutembea na mwanamke ni mama Zuuh sasa hivi. Kwa mipango ya mwenyezi Mungu nikamfanya mjamzito. Akaniambia na kuniuliza ikiwa niko tayari ama atoe. Kwa kuwa mimi ni Muislamu, kuutoa mimba ni kushiriki  dhambi.  Sikuwa tayari kwa hayo. Niliamua ni njia ambayo mwenyez Mungu aliamua kunipitisha" Harmonize alisema.

Alisema  kuwa Sarah aliumia sana moyoni baada ya kupata habari kwamba alikuwa amecheza karata nje na kupachika mwanadada mwingine ujauzito.

Alieleza kuwa  alijaribu sana kumshawishi mpenziwe amsamehe ili warejeshe mahusiano yao ila juhudi zake zote ziliangulia patupu.

"Ilimuumiza sana Sarah kwa sababu mnapokuwa na mtu kwenye mahusiano mnakuwa na ndoto za kupata familia bora. Ilimuumiza sana na akashindwa kukubali. Kwa kipindi kirefu nilikuwa nikificha  almaradi tu mahusiano yetu yaweze kuenda vyema. Nilikuwa naamini ingawa alikuwa na hasira wakati ungefika akubali matokeo. Nilikuwa natafuta njia zingine za kuenda kwake ili awe sawa na yote lakini kwa bahati mbaya ilishindikana hakuweza kukubali na akaenda"  alisimulia.

Ziara ya Sarah nchini Tanzania inakuja wakati mahaba Harmonize na mchumba wake wa sasa Kajala Masanja yakiwa yamenoga. Wawili hao ambao walikuwa wametengana mwaka jana walirudiana miezi kadhaa iliyopita na tangu wakati huo wamekuwa wakitia juhudi kubwa katika kuboresha mahusiano yao.