Simba mawindoni! Diamond Platnumz anamsaka Baby Mama mwingine

Muhtasari

•Baba huyo wa watoto wanne wanaojulikana amesema kuwa wakati umewadia kwake kuongeza mtoto mwingine.

•Mwanamuziki huyo tayari ana watoto wanne wanaojulikana wazi ambao alipata na wanawake watatu tofauti.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo Diamond Platnumz amedokeza kuwa yupo mbioni kumtafuta mwanamke atakayemzalia mtoto mwingine.

Baba huyo wa watoto wanne wanaojulikana amesema kuwa wakati umewadia kwake kuongeza mtoto mwingine.

Diamond alifunguka hayo wakati akirejelea video ambayo ilimuonyesha akinengua kiuno huku wimbo wake 'OKA' ukicheza.

"Unajua ni wakati wa kuongeza mtoto mwingine. Nawavutia kina mama," Alisema.

Alikuwa anamjibu shabiki aliyehoji "Kwa nini unacheza na shinikizo la damu ya watu siku ya Jumatatu, ni haki?" chini ya video hiyo.

Katika video hiyo Diamond alionekana akicheza densi bila shati ndani ya chumba cha kufanyia mazoezi.

Chini ya video hiyo, bosi huyo wa WCB alifichua kuwa huwa anachelewa kutoka GYM akinengua kiuno.

"Ikiwa unashangaa mbona huwa nachukua muda mrefu ndani ya GYM #OKAchallenge ft mbosso," Aliandika.

Mwanamuziki huyo tayari ana watoto wanne wanaojulikana wazi ambao alipata na wanawake watatu tofauti.

Diamond alipata watoto wawili na mwanasoshalaiti kutoka Uganda, Zari Hassan. Wawili hao walichumbiana kwa muda mrefu kati ya 2014 na 2017.

Tiffah Dangote ambaye ni mtoto wa kwanza wa Diamond na Zari alizaliwa mwaka wa 2015 huku kaka yake Prince Nillan akizaliwa takriban mwaka mmoja baadae.

Mwanamuziki huyo alipata mtoto wake wa tatu na mwanamuziki Hamisa Mobetto ambaye alichumbiana naye kwa kipindi kifupi.  Dylan Abdul Naseeb alizaliwa mwaka wa 2017.

Oktoba 2019 Diamond alipata mtoto mwingine, Naseeb Junior na mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna. Wawili hao walitengana miezi michache baadae ila wanaendelea kushirikiana katika malezi.

Licha ya kutengana na mama zai, Diamond amekuwa akiwasherehekea na kuwashughulikia watoto wake. Hata hivyo kumekuwa na tetesi kuwa anawapendelea watoto wake wawili na Zari zaidi ya hao wengine wawili.