"Sisi ni wadogo sana kuwa na mtoto sekondari, arudie!" Samidoh, Edday walalamika binti yao kuingia Sekondari

Wakati akitoa hoja yake kuhusu wao kuwa wadogo sana kuwa na mtoto Sekondari, Edday alimtambua Samidoh kama mume wake.

Muhtasari

•Samidoh na Edday walitania kuwa hawakukubali kuwa na mtoto katika shule ya Sekondari na kumtaka binti yao kurudia darasa la nane.

•"Nataka kusisitiza hii stori, hakuna vile tunaweza kuwa na mtoto katika shule ya sekondari. Sisi ni wadogo sana!," Edday alisema.

Samidoh, Edday na watoto wao
Image: INSTAGRAM// SAMIDOH

Wazazi wenza Samidoh Muchoki na Edday Nderitu walilalamika kwa mzaha baada ya binti yao mzaliwa wa kwanza, Shirleen Muchoki kuhitimu kutoka Shule ya Msingi na kujiunga na shule ya Upili.

Shirleen ambaye pia alifikisha umri wa miaka 14 hivi majuzi alimaliza darasa lake la nane katika shule moja nchini Marekani na wazazi wake waliungana tena kumsherehekea.

Katika video iliyoshirikishwa na kaka wa Samidoh, Waweru Uyu, wazazi wenza hao wawili ambao wamekuwa wakiishi mbali na mwingine kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita walitania kuwa hawakukubali kuwa na mtoto katika shule ya Sekondari na kumtaka binti yao kurudia darasa la nane

“Tumeamua hivi, sisi ni watu wadogo sana kuwa na mtoto katika shule ya upili. Arudie,” Samidoh alisema huku akimshika Edday shingoni.

Edday pia alisisitiza kuhusu hisia za mzazi mwenzake akisema kwamba wao ni wadogo sana kuwa na mtoto katika shule ya upili.

Huku akieleza hoja yake, mama huyo wa watoto watatu pia alionekana kuthibitisha kuwa staa huyo wa Mugithi bado ni mume wake.

"Nataka kusisitiza hii stori, hakuna vile tunaweza kuwa na mtoto katika shule ya sekondari. Sisi ni wadogo sana!," Edday alisema.

Huku akimuangalia mzazi mwenzake Samidoh, alisema, “Kama mume wangu anavyosema…, tuangalieni, angalia nyuso zetu.”

Katika video hiyo ambayo ilirekodiwa katika sehemu iliyoonekana kuwa hoteli,  wazazi hao wawili walionekana kuwa na furaha pamoja na kushikana kama watu wanaopendana.

Hii imeibua tena maswali tata kuhusu hali halisi ya ndoa ya wazazi hao wawili ambao waliishi pamoja kwa zaidi ya muongo mmoja hadi mwaka jana wakati ambapo Edday pamoja na watoto wao watatu walihamia Marekani na kumuacha Samidoh nchini Kenya.

Bi Edday Nderitu kwa sasa anaishi Marekani pamoja na watoto wao watatu.  Aliondoka nchini mapema mwaka jana na anaonekana tayari kutulia huko vizuri huku watoto wakiwa wameanza shule huko.

Mwezi Julai mwaka jana, Bi Edday Nderitu aliweka wazi kwamba alimuacha mumewe ili awe na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.

Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."