"Siwezi kutembea vizuri!" Ex wa Eric Omondi avunja kimya baada ya kudhulumiwa na mpenziwe

Muhtasari

•Chantal Grazioli amedai kwamba sasa hawezi kutembea vizuri kufuatia vurugu alizokabiliana nazo.

•Chantal amemshukuru Eric kwa kujitolea kumsaidia na kuweka hadharani yale ambayo amekuwa akipitia.

Eric Omondi na Chantal Grazioli
Eric Omondi na Chantal Grazioli
Image: ERIC OMONDI SOCIAL

Bi Chantal Grazioli amethibitisha kuwa mpenzi wake Nicola Traldi alimshambulia na kumsababishia majeraha mwilini. 

Mpenzi huyo wa zamani wa Eric Omondi amedai kwamba sasa hawezi kutembea vizuri kufuatia vurugu alizokabiliana nazo.

"Niliona watu wengine wakichukulia hii kama mzaha. Sio mzaha! Siwezi kutembea vizuri nimejeruhiwa na kuvunjika," Chantal alisema kupitia mtandao wa Instagram.

Mnamo Ijumaa Eric alisema kuwa mpenzi huyo wake wa zamani alimpigia simu mwendo wa saa mbili asubuhi kumwarifu jinsi mpenzi wake alivyomshambulia.

Alieleza kuwa alikimbia kwa Chantal punde baada ya kupokea taarifa hiyo na kumkuta akiwa katika hali mbaya.

"Nilipata Chantal amevunjika mguu. Alikuwa amenyongwa kwa shingo. Alikuwa ameangushwa kwa ngazi. Vitu vilikuwa vimepasuka. Ni mlinzi, majirani na caretaker ambao walimsaidia," Alidai Eric.

Mchekeshaji huyo alipakia video iliyoonyesha Chantal akichuchumia kwa uchungu huku akiwa na matone ya damu kwenye mguu.

Wanamitandao walifurika chini ya chapisho la mchekeshaji huyo kwenye Instagram na kutoa hisia tofauti. Ingawa wengi walionekana kukemea tukio hilo, baadhi walieleza shaka yao huku wakidai kuwa wawili hao walikuwa wanatafuta kiki tu.

Katika taarifa yake, Chantal amemshukuru mpenzi huyo wake wa zamani kwa kujitolea kumsaidia na kuweka hadharani yale ambayo amekuwa akipitia.

"Vurugu sio kitu cha kuchukuliwa kirahisi au kuchezewa, kuna watu ambao wanaipitia na ninamshukuru Eric kwa kuizungumzia na kuchukua muda kuipitia," Alisema.

Ijumaa Eric alichukua hatua ya kufika katika kituo cha polisi kuripoti mpenzi wa sasa wa Chantal kwa madai ya dhuluma.

Bw Traldi hata hivyo tayari amejitokeza kupuuzilia madai hayo na kusisitiza kuwa hana hatia yoyote.

Huku akijitetea, Traldi alisema madai ya Eric si ya kweli huku akidai kuwa hana uwezo wa kupiga mwanamke. 

"Nimesingiziwa kwa jambo ambalo singefanya kamwe, lisilosemeka, Ni siku ya huzuni.. Nisingewekelea mikono yangu juu ya mwanamke. Mimi ni baba wa mabinti wawili. Ukweli utajulikana," Traldi alisema kupitia Instagram.