Sonko adai ndiye alimshauri Karen Nyamu amfuate Samidoh Marekani, aeleza kwa nini

Kumekuwa na madai kuwa Karen anakaa pamoja na Samidoh na hata wanagawana mavazi.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watatu alithibitisha hayo siku ya Jumatano kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

•Sonko alidai kwamba alimdokezea Karen kuwa kuna baridi kali Marekani na kumuonya kuwa huenda  Samidoh akaanguka kwenye majaribio.

Mike Sonko, Karen Nyamu, Samidoh
Image: FACEBOOK

Wakili na seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu yupo nchini Marekani.

Mama huyo wa watoto watatu alithibitisha hayo siku ya Jumatano kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

"Huku yuwes (USA)," aliandika chini ya picha aliyopakia Facebook.

Kumekuwa na madai kuwa seneta huyo alisafiri hadi Marekani wiki jana ili kuungana na mzazi mwenzake, Samidoh. Wawili hao ambao wana watoto wawili pamoja, Samuel Muchoki Jr na Wairimu wanaaminika kuwa kwenye mahusiano.

Samidoh, staa maarufu wa Mugithii,  amekuwa kwenye safari ya muziki nchini Marekani kwa siku kadhaa zilizopita na amekuwa akichapisha baadhi ya kumbukumbu ambazo ameweza kunasa katika ziara hiyo.

Wapelelezi wa mitandaoni wameweza kubaini kuwa wazazi wenza hao huenda wanakaa pamoja Marekani huku ikidaiwa kuwa hata koti ambayo Karen alikuwa amevaa katika picha aliyopakia ni ya mwimbaji huyo.

Katika sehemu ya maoni ya chapisho la Facebook la Bi Karen, aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko aliibua madai kuwa yeye ndiye aliyemshauri kumfuata mwimbaji huyo wa Mugithi nchini Marekani.

Sonko ambaye kwa sasa amejikita katika biashara alidai kwamba alimdokezea Karen kuwa kuna baridi kali Marekani na kumuonya kuwa huenda mzazi mwenzake Samidoh akaanguka kwenye majaribio.

"Si nilikuambia ukimbie huko kwa mzee kuna baridi, huko yani baridi inakuja na barafu mtu hawezi akalala kitandani pekee yake," alisema.

Aidha, gavana huyo wa zamani alimuonya Karen kuwa mzazi mwezake alikuwa karibu kutekwa na mwanamke mwingine.

Takriban mwezi mmoja uliopita Sonko alidai kwamba ndiye aliyemuunganisha Karen Nyamu na Samidoh. Alidai kuwa  aliwaunganisha wazazi wenza hao katika hafla ya Mugithi Night iliyofanyika Dubai miaka kadhaa iliyopita.

Mwanasiasa huyo alikuwa akitoa maoni yake chini ya chapisho  la Karen kwenye Facebook wakati alipotoa ufichuzi huo.

"Mnafaa mniitie chai. Mimi ndio nilikupea Samidoh pale Dubai nikiwa na Moses Kuria wakati wa Mugithi night," alimwambia Karen.

Karen ambaye kwa sasa ana watoto wawili pamoja na Samidoh hakupinga kauli hiyo na badala yake akamuomba asifichue zaidi.

"Mdosi malizia tu hapo usitoe video," alimjibu Sonko.

Katika mahojiano ya hapo nyuma na Radio Jambo, Karen alifunguka kuhusu kukutana kwake kwa mara ya kwanza na msanii huyo ambapo baadae alipakia video iliyoonyesha wakijivinajiri na ikikosolewa sana mtandaoni.

Wakati huo alikana kuwa kwenye mahusiano naye na kusema kuwa uhusiano wake na Samidoh haukuwa wa kimapenzi.

"Samidoh ni rafiki yangu. Nilidhani nilichapisha tu video kama vile unavyochapisha video za marafiki zako wengine. Walakini, watu walianza kutoa maoni tofauti, kama kuhusu mke wa Samidoh, na kwa hivyo niliamua kuifuta. Sikuwa na nia yoyote mbaya, tena Samidoh ni chapa yake mwenyewe, na sikutaka kuichafua. Tulikuwa Dubai ambapo Sonko na wanasiasa wengine walikuwa pia, na tulikuwa tukikaa karibu na eneo moja, na tulipanda mashua pamoja kama marafiki," alisema.

Licha ya awali kukana kuwa kwenye mahusiano wawili hao walibarikiwa na mtoto wa kiume pamoja mnamo Novemba 2020. Karen alithibitisha Samidoh kuwa baba ya mwanawe mwezi Februari mwaka jana.