Stivo Simple Boy asimulia jinsi alivyotiwa mbaroni kwa madai ya ubakaji

Muhtasari

•Stivo alikamatwa baada ya mwanadada mmoja ambaye alikuwa anammezea mate kumshtumu kwa ubakaji.

•Mwanamuziki huyo pia alidai kuwa alinyanyaswa wakati alipokuwa amezuiliwa ndani ya seli ya polisi.

Image: INSTAGRAM// STIVO SIMPLE BOY

Stivo Simple Boy amefunguka kuwa amewahi kukamatwa na kuzuiliwa korokoroni kwa kipindi cha wiki moja.

Mwanamuziki huyo amedai alitiwa mbaroni baada ya mwanadada mmoja ambaye alikuwa anammezea mate kumshtumu kwa ubakaji.

"Huyo msichana alikuwa rafiki yangu. Kumbe alikuwa ananimezea mate na hataki kuniambia. Ilibidi sasa aseme uwongo," Stivo alisimulia katika mahojiano na Oga Obinna.

Msanii huyo kutoka mtaa wa Kibera alifichua kuwa alikuwa rafiki wa karibu wa familia ya mwanadada aliyedai kuwa alimbaka.

"Mama akawa mkali akitaka kujua kama ni kweli nilimbaka . Nilishikwa tukaenda kupimwa," Alieleza. 

Vipimo vya hospitali hata hivyo zilifutilia mbali madai hayo kwani vilibainisha kuwa mlalamishi hakubakwa.

Stivo alisema alizuiliwa katika kituo cha polisi kwa wiki moja kabla ya matokeo ya hospitali kutoka.

"Nililala ndani wiki moja huku kesi ikiendelea. Nilipotoka waliomba msamaha mambo yakawa sawa," Alisema Stivo.

Mwanamuziki huyo pia alidai kuwa alinyanyaswa wakati alipokuwa amezuiliwa ndani ya seli ya polisi.

Vilivile alifichua kuwa amewahi kufikishwa mahakamani baada ya vifaa vya ujenzi kuibiwa katika mjengo aliokuwa analinda.

"Mwizi alikuja kuiba chuma na mimi sikujua. Nilikuwa napiga patrol. Mwenzangu alikuwa amesinzia. Niliamua kuingia msalani, kumbe hapo wizi ilikuwa inaendelea," Alisimulia.

Siku iliyofuata alipofika kazini alikamatwa pamoja na mwenzake na kufikishwa mahakamani  kwa madai ya wizi. Rafiki yake alifungwa kifungo cha miaka miwili ila yeye akanusurika na kuenda nyumbani.