"Tafadhali niombeeni!" Mejja afichua tatizo la afya la kutisha analopambana nalo

Mwimbaji huyo alidokeza kwamba anahisi kama kwamba sauti yake imebadilika.

Muhtasari

•Mejja alifichua kwamba hajaweza kuachia kibao chochote mwaka huu kwa kuwa amekuwa akipambana na tatizo la koo.

•Mejja alidokeza kwamba tatizo lake lilisababishwa na kunywa vitu vingi vya sukari na kutokunywa maji kwa wingi.

•Mejja alidokeza kwamba tatizo lake lilisababishwa na kunywa vitu vingi vya sukari na kutokunywa maji kwa wingi.

Image: INSTAGRAM// MEJJA

Mwimbaji mashuhuri Major Nameye Khadija almaarufu Mejja ameeleza sababu ya ukimya wake mkubwa katika siku za hivi karibuni.

Katika mahojiano na Willy M. Tuva, mwanamuziki huyo ambaye amekuwa akitumbuiza kwa zaidi ya mwongo mmoja alifichua kwamba hajaweza kuachia kibao chochote mwaka huu kwa kuwa amekuwa akipambana na tatizo la koo.

Alidokeza kuwa tatizo hilo lilianza alipokuwa ameenda kutumbuiza nchini Australia mwaka jana lakini hakuweza kupata dawa mara moja.

"Vile nilirudi Kenya nilikuwa naskia hiyo uchungu ilikuwa inakuja inapotea.Kama Mkenya wa kawaida nikaenda kwa duka la dawa. Nilichukua dawa ambayo nilipatiwa. Kweli dawa nilipona lakini sio sana, nikienda kama siku tatu hivi, nikipigwa na baridi tatizo linarudi. Bado nilikuwa napuuza," Mejja alisema.

Mejja alifichua kuwa tatizo lake iliendelea hadi mwaka huu na hata likaongezeka hadi akaamua kwenda hospitalini.

"Katika ile harakati ya kutaka kutoa kikohozi, nilikuwa naona madoa ya damu. Hapo ndio nikajua kuna shida nikaenda hospitali," alisema.

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa madaktari walimchambua koo na kugundua kwamba alikuwa na tatizo lilihohitaji kushughulikiwa.

"Niliambiwa nikae kama mwezi mmoja hivi bila kutumia sauti yangu sana. Niliambiwa nisiongee sana na nisitumbuize. Pia niliambiwa niende kwa matibabu ya usafi wa sauti. Sasa naenda matibabu," alisema.

Mwanamuziki huyo alidokeza kwamba tatizo lake lilisababishwa na kunywa vitu vingi vya sukari na kutokunywa maji kwa wingi.

Pia alidokeza kwamba anahisi kama kwamba sauti yake imebadilika huku akieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali hiyo. 

"Naomba mashabiki waniombee. Inaniathiri kisaikolojia. Napenda muziki sana, ni kila kitu kwangu. Kweli inanisumbua sana. Naweza taka watu waniombee, ukifanya sala yako tafadhali nikumbukeni," alisema.

Mejja pia aliwatahadharisha Wakenya dhidi ya kunywa vinywaji vyenye sukari nyingi na kuwashauri wanywe maji kwa wingi.