Terence Creative hatimaye avunja kimya kuhusu mkewe kumrombosea Bahati

Diana Marua alikuwepo wakati mumewe alikuwa akijivinjari na Bi Chebby.

Muhtasari

•Terence aliweka wazi kuwa hana shida yoyote na mkewe kucheza densi na mwanamume mwingine.

•Terence alibainisha kuwa wakati tukio hilo linatokea mkewe Bahati, Diana Marua bado hakuwa mjamzito

Terence Creative na mkewe Milly Chebby
Terence Creative na mkewe Milly Chebby
Image: Terence Creative//Facebook

Mchekeshaji Lawrence Macharia almaarufu Terence Creative hatimaye amejibu baada ya video inayomuonyesha mkewe Milly Chebby akisakata densi tatanishi na Bahati kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

 Hivi majuzi, video ya zamani ya Milly akimrombosea mwimbaji wa zamani wa nyimbo za injili Bahati iliibuka mitandaoni na kuzua mjadala mkubwa. Wanamitandao wengi walijitokeza kutoa hisia mseto huku baadhi wakikosoa kitendo cha wasanii hao wawili ambao tayari wapo kwenye ndoa tofauti.

Katika mahojiano ya simu na kituo kimoja cha redio cha hapa nchini, Terence aliweka wazi kuwa hana shida yoyote na mkewe kucheza densi na mwanamume mwingine na kufichua kuwa hata mkewe Bahati, Diana Marua alikuwepo wakati hayo yalifanyika na wote walifurahia kutazama.

"Kuna shida gani? Sijalazwa hospitali popote. Nipate wivu wa nini?. Yeye anachemsha maji mimi nayaogea. Pia mimi namchemshia naye anaoga kwake," alisema.

Baba huyo wa watoto watatu alibainisha kuwa wakati tukio hilo linatokea mkewe Bahati ambaye anatarajia kujifungua hivi karibuni hata bado hakuwa amepata ujauzito wa mtoto wake wa tatu.

"Hiyo ni video ya kitambo sijui mbona imeletwa mitandaoni sasa hivi. Pia mimi nilikuwa pale. Tuko sawa kabisa," alisema Terence.

Katika video iliyosambaa mitandaoni, Bahati na Milly Chebby walionekana wakijivinjari mbele ya watazamaji kadhaa waliokuwa nyuma ya camera ambao waliwashangalia kwa sauti. Diana Marua ni miongoni mwa waliokuwa wakishangilia wakati mumewe akishiriki kipindi kizuri na mkewe Terence.

Mbali na kuwa wasanii wenza, wanandoa Terence Creative na Milly Chebby ni marafiki na wanandoa Bahati na Diana Marua.

Soma baadhi ya maoni ya wanamitandao kuhusu video hiyo:-

m.currie sio suala kubwa mradi hawajashikana nyama kwa nyama.

terrymuthama Inafanyika tu kwa watu wenye pesa. sisi wengine tukijaribu tanapewa onyo

tallman_kenya Hakuna mipaka iliyovukwa

yvessricky Vile mimi huwa na wivu hapo ndio urafiki unaishia.