Tusi kwa Diamond? Zari na mpenzi wake washabikia kazi ya Harmonize

Hii ni mara ya pili wiki hii ambapo mzazi huyo mwenzake Diamond ametumia wimbo wa Harmonize.

Muhtasari

•Zari kwa mara ya nyingine katika muda wa siku chache ametengeneza video ya Tiktok akitumia wimbo mpya wa Harmonize ‘Single Again’.

•Zari alionekana kutoa tahadhari kuwa sababu tu alifanya challenge ya 'Single Again' haimaanishi kwamba hayuko kwenye mahusiano 

Zari Hassan, Shakib Cham na Harmonize
Image: INSTAGRAM//

Mwanasosholaiti maarufu wa Uganda, Zari Hassan, kwa mara ya nyingine katika muda wa siku chache ametengeneza video ya Tiktok akitumia wimbo mpya wa staa wa Bongo, Harmonize ‘Single Again’.

Siku ya Alhamisi, mke huyo wa zamani wa wa bosi wa WCB Diamond Platnumz kwenye ukurasa wake wa Tiktok alichapisha video yake na mpenzi wake wa sasa, Shakib Lutaaya  wakisafiri kwenye gari lao.

Kwenye video hiyo, Shakib hakuonekana kuwa na furaha huku mama huyo wa watoto watano akimrekodi wakati akiendesha gari.

“Aaiii mbona amekasirika lakini," Zari alihoji chini ya video hiyo.

Wimbo unaovuma wa Konde Boy 'Single Again' ulicheza wakati video hiyo ikiendelea kucheza.

Mwanasosholaiti huyo hata hivyo alionekana kutoa tahadhari kuwa sababu tu alifanya challenge ya 'Single Again' haimaanishi kwamba hayuko kwenye mahusiano kama watumiaji wengi wa Tiktok wanaofanya hivyo.

"Tafadhali, sio wanawake wote kwenye challenge hii wako single," alisema.

Harmonize ambaye bila shaka alifurahishwa na kitendo cha mpenzi huyo wa zamani wa hasidi wake mkuu, Diamond alichapisha tena video hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram kwa mashabiki wake kuona.

Mapema wiki hii, Zari ambaye  anaishi Afrika Kusini alitengeneza video nyingine akitumia wimbo wa mwimbaji huyo.

"Huyo Shangazi mmoja tajiri ambaye huwa anajigamba jinsi alivyoolewa na bilionea. Sasa amepewa talaka na prenup.. Kurudi kwenye nyumba ya familia,"  mwanasoshalaiti huyo aliandika kwenye video hiyo ambayo ilimuonyesha kama kwamba anarudi nyumbani kwao akiwa amevunjika moyo.

Harmonize alionekana wazi kufurahishwa video ya mwanasosholaiti huyo na hata akaichapisha  kwenye ukurasa wake wa Instragram.

Wakati huo, mwimbaji huyo wa bongo alikiri heshima yake kubwa kwa mfanyibiashara huyo ambaye kwa sasa anaishi Afrika Kusini.

"Nimeipost mara mbili kwa sababu ni boss lady. Heshima kubwa kwa bosi @zarithebosslady," Konde Boy  aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo ambayo kwa kawaida hutumika kuashiria upendo kwa mtu.

Kitendo hicho kilionekana kuwa chenye utata ikizingatiwa kwamba Zari ni mzazi mwenza wa mpinzani mkuu wa Harmonize kwenye tasnia ya Bongo, Diamond Platnumz. Ingependeza kuona jinsi Diamond anapokea hili.