"Ua nilipendalo zaidi" Juliani na mkewe Lilian Nganga washerehekeana kwa jumbe za kipekee

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo wa nyimbo za kufoka alimtaja Bi Lilian kama 'ua' lake alipendalo zaidi.

Juliani na mke wake Lilian Nganga
Juliani na mke wake Lilian Nganga
Image: HISANI

Wanandoa mashuhuri Juliani na Lilian Ng'ang'a wamezamia mitandaoni kusherehekeana na kuonyesha ulimwengu penzi lao.

Siku ya Jumanne, Juliani ambaye kwa jina halisi ni Julius Owino alipakia picha yake na mkewe na kuiambatanisha na ujumbe mtamu. Kwenye picha hiyo inayoaminika kupigiwa nyumbani kwa kina Juliani Kisumu, wawili hao walionekana wenye bashasha tele.

Mwanamuziki huyo wa nyimbo za kufoka alimtaja Bi Lilian kama 'ua' lake alipendalo zaidi.

"Ua nilipendalo zaidi ni Lily," Juliani aliandika chini ya picha yake na Lilian.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Lilian alipakia picha ya zilizoonekana kuwa pipi mbili za umbo wa moyo zilizokuwa na maandishi  'J' na 'L', kusimamia Juliani na Lilian.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NGANGA

Wanandoa hao wamekuwa wakiweka mahusiano yao bayana tangu mwezi Septemba, mwaka jana walipojitokeza kwa mara ya kwanza kutangaza kuwa wanachumbiana.

Wawili hao walifunga pingu za maisha mapema mwezi uliopita katika harusi iliyohudhuriwa na wanafamilia na marafiki wachache.

Kwa sasa, Lilian ambaye ni mke wa zamani wa gavana wa Machakos Alfred Mutua ni mjamzito na anatarajia mtoto wake wa kwanza na Juliani.