Watoto wa Zari na Diamond wadokeza wazi hawafurahishwi na mpenzi mpya wa mama yao

Tiffah alimkosoa mama yake kwa kujitosa kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

Muhtasari

•Tiffah Dangote na Prince Nillan walimlaumu mama yao kwa kuvunja mahusiano yake na Diamond miaka kadhaa iliyopita.

"Kwa nini uliivunja familia? Uko na mtu mwingine, unatumia muda wako naye, huna wakati na familia, hatumii wakati wako na baba!" Tiffah alilalamika.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Ni wazi kuwa watoto wawili wa mwisho wa mwanasoshalaiti Zari Hassan hawana upendo mkubwa kwa mpenzi wake mpya Shakib Cham.

Tiffah Dangote na kakake Prince Nillan walionyesha wazi kuwa hawako radhi na mama yao kuchumbiana na mpenziwe mdogo katika kikao cha familia walichoagiza wakati baba yao Diamond Platnumz alipowatembelea Afrika Kusini mapema wiki hii.

Katika kikao hicho, ndugu hao wawili walimlaumu mama yao kwa kuvunja mahusiano yake na Diamond miaka kadhaa iliyopita.

"Yeye (Zari) sasa yuko na mtu mwingine, nasema ukweli," Tiffah alimwambia Diamond.

Huku akimuunga mkono dada yake, Prince Nillan alisema, "Kwa hivyo Mama T (Zari) ndiye alivunja familia," 

Diamond kwa utani aliyaunga mkono maoni ya watoto wake kwamba mpenzi huyo wake wa zamani  ndiye aliyevunja familia.

Ndugu hao wawili wenye umri wa miaka 7 na 5 walikanusha madai kuwa baba yao yuko katika mahusiano na mwanamke mwingine. Pia walikana madai ya mama yao kuwa Diamond yuko na watoto wengine kando yao.

"Siamini una mpenzi mwingine siamini una watoto wengine," alisema Tiffah.

Tiffah aliendelea kumlalamikia mama yake kwa kuvunja familia huku akimkosoa kwa kujitosa kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

Pia alimshtumu kwa kutumia muda wake mwingi na mpenzi wake na kukosa muda wa kuwa na baba yao wampendaye.

"Kwa nini uliivunja familia? Uko na mtu mwingine, unatumia muda wako naye, huna wakati na familia, hatumii wakati wako na baba!" alimlalamikia mamake.

Diamond ambaye alishangazwa sana na hisia za watoto wake alidokeza kuwa watakapokuja kubaini ukweli hatimaye "watamshambulia."

Licha ya kufurahishwa na wanawe kwa kutomshtumu kwa kusababisha kuvunjika kwa familia, staa huyo hata hivyo alimtetea mzazi huyo mwenzake kwa watoto wao na kuwahakikishia kuwa familia bado ipo imara.

"Mkimuona na mtu mwingine anaigiza tu. Kama vile tu huwa mnaona nikifanya katika video za muziki." aliwaambia.

Zari ambaye alikuwa akifuatilia kwa makini wakati watoto wake wakiibua madai mazito dhidi yake alionekana kushangazwa na jinsi walivyogeuza kidole cha lawana kutoka kwa mpenzi huyo wake wa zamani na kuelekeza kwake.