"Watu hurudi kuangalia kama bado wewe ni mjinga!" Kajala azima juhudi za Harmonize

Muhtasari

•Kajala amekuwa akipakia jumbe za kimafumbo ambazo zimeonekana kuelekezwa kwa Harmonize.

•Ametahadharisha watu dhidi ya kupenda sana huku akiwasihi wakumbuke yaliyowahi kuwatendekea hapo awali.

Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masanja
Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masanja
Image: HISANI

Muigizaji Fridah Kajala Masanja amekuwa bizi sana kwenye mtandao wa Instagram hasa tangu aliyekuwa mpenzi wake Harmonize aanze juhudi za kufufua mahusiano yao.

Kuelekea mwishoni mwa mwezi Machi, Harmonize alitangaza kutengena kwake na Briana na kudai roho yake yamtamani Kajala tu.

Staa huyo wa Bongo alikiri kuwa hakuwahi kuweza kumsahau Kajala baada ya kutengana naye, jambo ambalo alihisi lilitatiza mahusiano yake na Briana.

"Sina tatizo na Briana. Yeye ni mtu mzuri ila hatuko pamoja kwa sababu, moja nilimwambia nimetengana na mtu bila kugombana na nampenda sanaa sasa sina uhakika kama nimemove on, lolote linaweza kutokea," Harmonize alisema.

Harmonize alianza juhudi za kumshawishi mpenzi huyo wake wa zamani warudiane huku akipiga hatua kama kumuomba msamaha, kuweka bango lao barabarani na kumnunulia zawadi za thamani.

Mapema mwezi Aprili Kajala alionekana kuvunja kimya chake na kumjibu mwanamuziki huyo kwa njia ya mafumbo.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni ujumbe wa moja kwa moja kwa Harmonize, mwigizaji huyo alijirekodi akiwa ndani ya gari yake huku akiimba wimbo wa Rayvanny na Zuchu 'I miss you'. (Nakupeza) na kuweka video hiyo kwenye Instastori zake.

Kajala alichagua kupakia  kipande cha wimbo huo kinachosema, "Sipendi Tuchukiane,Japo Najua Mungu Amenilinda Na Mengi.Na sisemi Turudiane,Hilo Tambua Mie Nilipovunja,Sijengi Na Niliko Salama"

Tangu wakati huo mama huyo wa binti mmoja amekuwa akipakia jumbe za kimafumbo ambazo zimeonekana kuelekezwa kwa Harmonize.

Kupita Instastori zake Kajala amechapisha "Wakati mwingine watu hurudi katika maisha yako kuangalia kama bado wewe ni mjinga."

Ujumbe huo umeonekana kuwa mojawapo wa majibu ambayo amekuwa akimpatia bosi huyo wa Kondegang kwa njia fiche.

Kajala pia ametahadharisha watu dhidi ya kupenda sana huku akiwasihi wakumbuke yaliyowahi kuwatendekea hapo awali.

" Usikubali kushikamana sana kumbuka kilichotokea mara ya mwisho..." Aliandika katika chapisho lingine la Instagram.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa jumbe zake zinazungumzia jambo ambalo Harmonize amekuwa akijaribu kufanya, kurejesha mahusiano yao.