Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Wilson Abubakar Radido almaarufu Willy Paul alivunja mtindo wake wa kawaida siku ya Jumapili, Januari 28 na kwenda kanisani kwa mara ya kwanza baada ya takriban miaka saba.
Katika taarifa yake Jumatatu asubuhi, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alifichua kwamba mara ya mwisho alihudhuria ibada ya kanisa tena ilikuwa mwaka wa 2017.
Alibainisha kwamba amekuwa akiepuka nyumba ya Mungu kwa miaka kadhaa iliyopita baada ya jambo ambalo hakupenda kumtokea hapo awali.
"Sijaenda kanisani tangu 2017, kwa sababu kanisa lilinifanyia kitu kibaya," Willy Paul alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Hata hivyo, alifichua kwamba alijisikia vizuri baada ya kuacha ya ndwele yapite na kuhudhuria ibada ya kanisa jijini Nairobi siku ya Jumapili.
“Lakini jana nilihudhuria ibada ya kanisa huko Embakasi na ninahisi faraja sana. Utakuwa mwaka mzuri sana kwa sababu nimeanza wangu kanisani,” alisema.
Mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi aliyezingirwa na utata mwingi hata hivyo aliambatanisha taarifa yake na picha ambayo haihusiani kabisa na kanisa. Ilikuwa ni picha yake akiwa na mwanamke mmoja kwenye kile kilichoonekana kama eneo la burudani.
Miaka kadhaa iliyopita, Willy Paul aliwashangaza Wakenya alipochukua hatua ya kuacha injili na kujiunga na tasnia ya muziki wa kilimwengu.
Mwaka wa 2021, alifunguka kwamba aligura tasnia ya muziki wa injili kwa sababu ya nguvu zisizoonekana ambazo zilifanya kazi usiku na mchana kumshusha. Hii ilisababisha msongo wa mawazo na mwishowe akavunjika.
Kwa maneno marefu, Willy Paul alielezea sababu yake kujiondoa kwenye muziki wa injili.
"Kama mpaka leo sijawai enda chini juu ya chuki basi sidhani kama nitawahi. Wengine mnaniuliza kwanini niliacha Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo... na hata kuniita majina kwa sababu simsifu tena Yesu nyimbo zangu. Kulingana na wao mimi ni mbaya sana na kila kitu kibaya.
Hao ndio watu wale wale walionipigania nikiwa upande wa Yesu 😆 Sababu za kwa nini niliondoka. Chuki kutoka kwa wasanii wenzangu na ma-DJ, nyimbo zangu kukosa kuchezwa hewani (kwa madai kwamba maudhui yangu hayakuwa ya Uungu wakati huo) ubaguzi na mapendeleo.
Nilikuwa msanii mkubwa lakini watu hawa waovu hawakuweza kuona hilo. Au walichagua tu kupuuza ukweli! Watu hawa walinivunja moyo! Waliniumiza sana, nilishuka moyo kwa muda wa miezi 4 niliendelea kulia kimya kimya kila siku moja na usiku. Ilifika mahali sikuweza kuvumilia tena... sikuwa na pesa za kulipia bili zangu na hata kusaidia pale nyumbani. Can you imagine I had the biggest songs na hawa watu wakanichorea hivo tu!” Willy Paul alilalamika.