"Yule kakosea, sikupendezwa!" Babake Diamond amkosoa kwa kutobolewa pua

Mzee Abdul alisema Diamond anapaswa kuangazia mambo mengine ya kujirembesha.

Muhtasari

•"Yule kakosea kweli. Kutokana na maadili yetu sisi, watoto wa kiume hawapaswi kufanya vitu kama hivyo," alisema.

•Mzee Abdul alisema ikiwa Diamond ataendelea na tabia zile huenda akapoteza mashabiki.

Diamond Platnumz, Mzee Abdul Juma Isack
Image: HISANI

Mzee Abdul Juma Isack amekosoa kitendo cha mwanawe Diamond Platnumz kutobolewa pua.

Wiki chache zilizopita, Diamond alichapisha video iliyoonyesha akitobolewa upande moja wa pua lake na kuwekwa herini. Hatua hiyo ilizua hisia mseto huku baadhi wakifurahishwa nayo na wengine wakimkosoa.

Mzee Abdul ambaye anaaminika kuwa baba mzazi wa staa huyo wa Bongo ameweka wazi kuwa jambo hilo halikumfurahisha.

"Yule kakosea kweli. Kutokana na maadili yetu sisi, watoto wa kiume hawapaswi kufanya vitu kama hivyo," alisema katika mahojiano na Mbengo TV.

Abdul alidai kuwa huenda mwimbaji huyo alichukua hatua hiyo kutokana na ustaa wake, utajiri, uwezo na kiburi.

Alisema Diamond anapaswa kuangazia mambo mengine ya kujirembesha bali na yanayokiuka maadili ya Kitanzania.

"Hayo sio maadili ya Kitanzania. Ni maadili ya mbali ya Kinyamwezi. Kusema kweli sikupendezwa na lile suala, aangalie kama kuna vitu vingine vya kugeza,"

Aidha alibainisha kuwa wasanii wengine wakubwa kama vile Ali kiba hawajaiga tabia kama za kujitoboa pua.

"Zamani tulikuwa na mitindo ya kujichorachora mwilini lakini sasa hivi tunajutia" alisema.

Amemshauri mwanamuziki huyo kutema mienendo isiyo ya kimaadili. Alisema ikiwa Diamond ataendelea na tabia zile huenda akapoteza mashabiki.

Abdul pia aliwaomba watu wa karibu na mwawe kumshauri kuhusu maadili mema.

Mzee Abdul alikiri kuwa muda mrefu umepita tangu alipomuona mwanawe kwa mara ya mwisho. Hata hivyo alieleza matumaini yake kuwa siku moja bosi huyo wa WCB atachukua hatua ya kumtembelea.

"Labda ana pilkapilka nyingi za kikazi. Labda anakosa kutulia akitafuta maisha. Ipo siku, kama ilivyotokea akanipa salamu, ipo siku atakuja kunipa salamu," alisema.

Mzee Abdul anaaminika kuwa baba mzazI wa Diamond. Hata hivyo, takriban miaka miwili iliyopita, familia ya Diamond ikiongozwa na mama yake Mama Dangote ilionekana kumkana na kujitenga naye.