•Zuchu alibainisha kuwa hata kabla hajaanza kutoka kimapenzi na bosi huyo wake, alifahamu fika kuwa ana watoto na wazazi wenza.
•Pia alisema hakuona chochote cha kimapenzi kati ya Diamond na mwimbaji huyo wa Kenya cha kumfanya awe na wasiwasi.
Malkia wa muziki wa Tanzania Zuhura Othman almaarufu Zuchu ameweka wazi kuwa hakuona tatizo kwa mpenzi wake Diamond Platnumz kushirikiana na aliyekuwa mpenzi wake Tanasha Donna kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wao Naseeb Jr.
Akizungumza katika mahojiano na Wasafi Media, binti huyo wa Khadija Kopa alibainisha kuwa hata kabla hajaanza kutoka kimapenzi na bosi huyo wake, alifahamu fika kuwa ana watoto na wazazi wenza.
Zuchu alisema alifahamu kuwa wakati mwingine bosi huyo wa WCB angeungana tena na wazazi wenzake na watoto wake katika hafla maalum na akaweka wazi kuwa alikuwa tayari kwa hilo.
“Mimi kipindi naanzana naye nilijua ana watoto kusema kweli. Nilijua ni lazima ashiriki kwenye vitu vya watoto wake. Kiuhalisia ukifuatilia sana vuta nikuvute za mitandao hutaishi maisha yako ya uhalisia na ukweli,” Zuchu alisema.
Aliongeza, “Naseeb ana watoto na kila siku itakuwa kwenye maisha ya watoto wake na watacelebrate birthdays, watakuwa na sikukuu na ni lazima wazazi wenza wote wawepo. Wale wameshakuwa familia mpaka mmoja wao azikwe. Na hata mmoja wao akizikwa lazima bado watakuwa wanafamilia.”
Mwimbaji huyo wa kibao ‘Sukari’ alibainisha kuwa wazazi wenza hao wawili kuungana tena kwa ajili ya siku ya kuzaliwa ya mtoto wao ni jambo la kawaida ambalo halikuhitaji kumfanya awe na wasiwasi.
Pia alisema hakuona chochote cha kimapenzi kati ya Diamond na mwimbaji huyo wa Kenya cha kumfanya awe na wasiwasi.
“Sikuona kitu chochote kibaya pale ambacho kilitokea. Sikuona kama wamekumbatiana, sikuona kama wamepigana mabusu. Yaani sikuona tatizo lolote, niliona tu wazazi wawili wamekutana kumsherehekea mtoto wao. Kwa hiyo wananchi huwezina nao watakushinda. Huwezi kupinga nao wana maneno mengi. Ni mambo ya kawaida,” alisema Zuchu.
Zuchu amepata dhihaka nyingi ndani ya takribani wiki mbili zilizopita tangu mpenzi wa zamani wa Diamond Platnumz, Tanasha Donna alipotua Tanzania kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wao Naseeb Jr.
Mwimbaji huyo wa Kenya kuonekana pamoja na Diamond na uhusiano wa karibu kati yake na aliyekuwa mama mkwewe, Mama Dangote uliwafanya wanamtandao kumtahadharisha Zuchu kuwa huenda mama huyo wa mvulana mmoja yuko mbioni kuchukua nafasi iliyokuwa yake.