Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amemtuliza mwanawe Prince Nillan baada ya kushindwa kuhudhuria sherehe ya siku yake ya kuzaliwa mnamo Jumatano, Desemba 6.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, bosi huyo wa lebo ya WCB alimtaka mtoto huyo wake wa pili wa mwanasosholaiti Zari Hassan asiwe na wasiwasi kuhusu yeye kutohudhuria sherehe yake kwani anapanga kulipa fidia.
Alisema ili kulipia kukosa karamu zilizopita, atawaandalia tafrija kubwa kijana wa miaka saba na dada yake mkubwa Tiffah Dangote.
“Nimekosa siku yako maalum na ya dada yako mwaka huu mwanangu.. Ila usijali, nitawafanyia wote Birthday Party maalum kwa ajili yako na dada yako mtakapokuja kwa ajili ya mkesha wa mwaka mpya nchini Tanzania!!!,” Diamond alisema kupitia Instagram.
Staa huyo wa bongo fleva aliendelea kumhakikisha mwanaye na Zari kuhusu upendo wake mkubwa kwake.
"Kumbuka Papa anakupenda sana @princenillan," alisema na kuambatanisha taarifa yake na picha ya mvulana huyo wa miaka saba.
Prince Nillan aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya saba siku ya Jumatano huku dada yake Tiffah Dangote akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 8 mnamo Agosti 6.
Wawili hao walikuwa nchini Tanzania kwa mara ya mwisho mwezi Oktoba ambapo walipata fursa ya kushiriki muda na familia ya Diamond.
Wawili hao ambao ndio watoto wakubwa wa bosi huyo wa WCB walisafiri naye Tanzania kutoka Afrika Kusini wanakoishi na mama yao.
Naseeb Jr, ambaye ni mtoto wa staa huyo na mrembo wa Kenya, Tanasha Donna, pia amekuwa akionekana na mwanamuziki huyo nchini Tanzania mara nyingi katika miezi kadhaa iliyopita na hata anaripotiwa kuanza masomo yake katika nchi hiyo jirani upande wa kusini mapema mwezi uliopita.
Wakati wa ziara ya Oktoba, Diamond alionyesha video nzuri ya wanawe hao watatu wakicheza pamoja. Pia alipakia video zaidi zake, watoto wake watatu na mama yake, Mama Dangote wakielekea uwanja wa ndege kwa gari lake la kifahari.
Msafara wa magari mengine ya kifahari yaliwasindikiza walipokuwa wakienda kupanda ndege yake binafsi kuwapeleka Kigali, Rwanda kwa ajili ya Tuzo na Tamasha la Trace.
“Kigali, Rwanda one time for the @traceawardsfestival,” Diamond aliandika chini ya video yake akiwa na watoto wake ndani ya ndege ambayo alipakia Instagram.