Siku chache tu baada ya kushtumiwa kukopi wimbo wa injili wa Kiswahili, lebo ya Diamond ya WCB imemulikwa tena kwa madai ya kukopi midundo na mawazo ya nyimbo za wasanii mbalimbali kwenye wimbo mpya wa Mbosso.
Ni wazi kuwa wimbo wa Mbosso akimshirikisha Diamond 'Yataniua' umefutwa kwenye mtandao wa YouTube kufuatia malalamishi ya hakimiliki. Wasanii hao wawili wanadaiwa kukopi maudhui kutoka kwa wimbo wa Asake 'Peace Be Unto You.'
Isitoshe, mastaa hao wawili wa bongo fleva pia wanadaiwa kukopi mawazo na midundo kutoka kwa wimbo wa Young Stunna 'Adiwele'.
Wakati Radio Jambo ilipochukua hatua ya kuangalia wimbo huo ulioachiwa hivi majuzi kwenye YouTube mnamo Jumamosi asubuhi tuligundua kwamba ulikuwa umezuiwa kwa sababu ya masuala ya hakimiliki.
"Video hii ina maudhui kutoka kwa Empire na Zikki Media Afrika Kusini, ambao mmoja au zaidi wameizuia kwa misingi ya hakimiliki," arifa iliyojitokeza kwenye mtandao wa Youtube kuhusu wimbo huo ilisoma.
Uchunguzi zaidi kutoka upande wetu ulibainisha kuwa kwa kweli kuna sehemu za wimbo 'Yataniua' zinazokaribia kufanana na nyimbo 'Adiwele' na 'Peace Be Unto You' ila tu lugha tofauti zimetumika kuimba.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya msanii mwingine wa WCB, Zuhura Othman almaarufu Zuchu kudaiwa kuiba baadhi ya mistari ya wimbo wake 'Kwikwi' kutoka kwa wimbo wa Enock Jonas 'Wema wa Mungu.'
Tarifa zilizopo ni kwamba malkia huyo wa Bongo alitumia kionjo pamoja na mtindo wa wimbo wa Jonas bila idhini.
Inaripotiwa kuwa kufuatia hayo Enock Jonas tayari amechukua hatua za kisheria na anadai kufidiwa milioni 500 (Ksh 25M) .
Bosi wa WCB, Diamond, mwenyewe amewahi kushtumiwa kwa kuiba ngoma za wenyewe. Miaka kadhaa iliyopita wakati yeye na timu yake ya Wasafi waliimba kibao kilichovuma cha ‘Zilipendwa’, msanii mkongwe wa Bongo H-Baba aliibuka na kudai kwamba wazo la kibao hicho lilikuwa lake.
H-Baba aliteta vikali kwamba Diamond alichukua kibao hicho kipindi wakiwa pamoja katika lebo ya Shawarbaru.
Hivi majuzi pia Diamond alisutwa vikali kwa kile mashabiki wa muziki walisema aliibamidundo ya ngoma ya msanii wa Kenya Otile Brown ‘Such Kinda Love’ na kuitumia katika kibao chake cha ‘Naanzaje’.