Diana Marua hatimaye ampa Bahati sababu kuu kwa nini hakutaka kuolewa naye

'Ulikuwa Bible, Bible, Bible, Bible. Nilikuwa nakuheshimu," Diana Marua alilalamika.

Muhtasari

•Diana alibainisha kwamba Bahati kuwa mdogo kwake kwa miaka mitatu kulimfanya aone kana kwamba hawakufaana.

•Diana alidokeza kwamba alipokutana kwa na mwimbaji huyo alikuwa mtakatifu sana, jambo ambalo hakuridhishwa nalo.

Bahati na mkewe Diana Marua
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwanablogu na rapa  Diana Marua amefichua kuwa moja ya sababu kwa nini alikuwa na shaka kuhusu kuolewa na Bahati ni tofauti zao za umri.

Akizungumza kwenye video ya hivi majuzi kwenye chaneli yake ya YouTube, mama huyo wa watoto watatu alisema kwamba matarajio  yake ya awali yalikuwa kuolewa na mwanamume ambaye ni mkubwa zaidi yake kiumri.

Diana alibainisha kwamba Bahati kuwa mdogo kwake kwa miaka mitatu kulimfanya aone kana kwamba hawakufaana..

"Sababu kuu ilikuwa umri. Wewe ni mdogo kuliko mimi kwa miaka mitatu. Jamii inaamini kuwa kama mwanamke huwezi kuchumbiana na mtu mdogo kuliko yeye. Ata mimi nilijua nikitaka kutulia nitatulia na mtu ambaye ana umri mkubwa kuniliko. Bora awe mkubwa kuniliko kwa mwaka mmoja tuko sawa,” Diana Marua alimwambia mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili kwenye video hiyo.

Wanandoa hao mashuhuri walikuwa wakizungumza kuhusu safari yao ya mahusiano na jinsi walivyoanza kuchumbiana.

Bahati ndiye aliyemuuliza mkewe kwa nini mwanzoni hakutaka kutulia naye kwenye ndoa.

“Tulipoanza kuchumbiana, mbona ulikuwa unaona kama siwezi kukuoa. Na sasa hivi uko hapa uko na watoto wangu nimekupea mimba moja, mbili, tatu, nne. Kwa nini uliona kama siwezi kukuoa,” Bahati alimuuliza mkewe.

Diana pia alidokeza kwamba alipokutana mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alikuwa mtakatifu sana, jambo ambalo hakuridhishwa nalo.

'Ulikuwa Bible, Bible, Bible, Bible. Nilikuwa nakuheshimu," Diana alisema.

Diana Marua alifichua kuwa baba wa watoto wake watatu hakujaribu kumtongoza walipokutana kwa mara ya kwanza. Wawili hao walianza kuchumbiana baadaye baada ya kukutana mara kadhaa na kujuana zaidi.

Mapema mwaka huu,  Diana alifichua hakuwa tayari kwa ndoa wakati alipokutana na mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili.

Akizungumza kwenye YouTube, mama huyo wa watoto watatu alidai kwamba Bahati alimnasa kwenye ndoa yao ya sasa.

Wanandoa hao walikuwa wanashiriki mazungumzo kuhusu maisha yao ya siku za nyuma wakati Diana Marua alipofichua kuwa Bahati alimpa ujauzito katika mwezi wa saba wa uchumba wao na kuwapelekea kwenye ndoa.

Ulininasa katika mwezi wa saba. Ulininasa. Lakini mpenzi ulikuwa unanipenda. Ulikuwa unakuja na hiyo Mercedes ya bluu kutoka Ruaka hadi Syokimau. Sijui mbona ulikuwa unakuja kwangu saa sita usiku," Diana alisimulia.

Kwenye mazungumzo hayo, Bahati alibainisha alimsaidia mwanavlogu huyo kuacha maisha ya anasa na kuanzisha familia.

"Kama isingekuwa mimi, zile klabu zinafungwa zingekuwa zinafungwa ukiwa ndani. Ungekuwa huko tu unaserereka unauliza utapata watoto lini alafu unajibu 'bado niko mdogo'" Bahati alimwambia mkewe.

Aliongeza,"Mimi ndio nilikwambia haya mambo ya kuwa mdogo."