DJ Fatxo azidiwa na hisia juu ya mapokezi ya muziki wa kwanza baada ya tuhuma za mauaji

Katika huo wimbo wa injili, mwimbaji huyo wa Mugithi alitoa ushuhuda wa yale ambayo amekabiliana nayo muda wa miezi mitatu iliyopita.

Muhtasari

•DJ Fatxo aliachia wimbo wa Injili wa Kikuyu  ‘Ngatho’ (Shukran) ambapo anamshukuru Mungu kwa kumsaidia kushinda yote aliyopitia na kumpa nafasi nyingine.

•Mapokezi ambayo wimbo huo wa dakika tano ulipata kwenye YouTube yalimshangaza mwimbaji huyo wa miaka 27 na hakuweza kuficha furaha yake.

Image: FACEBOOK// DJ FATXO

Siku ya  Jumanne, mwanamuziki Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo aliachia wimbo wake wa kwanza baada ya zaidi ya miezi sita.

Wimbo wa kurejea katika tasnia ya burudani wa mwimbaji huyo wa Mugithi ambaye amekuwa akipambana na tuhuma za mauaji katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ni wimbo wa Injili wa Kikuyu  ‘Ngatho’ (Shukran) ambapo anamshukuru Mungu kwa kumsaidia kushinda yote aliyopitia na kumpa nafasi nyingine.

“Nilikuwa nimetupwa mbali ili nisionekane.Lakini mikono yako Mungu ilinipokea. Jina langu lilikuwa likitajwa wanatoroka mbio, lakini Mungu ukanipa bega lako nililie hapo…,” DJ Fatxo aliimba katika wimbo huo.

Mapokezi ambayo wimbo huo wa dakika tano ulipata kwenye YouTube yalimshangaza mwimbaji huyo wa miaka 27 na hakuweza kuficha furaha yake.

"Wueh, nimezidiwa na hisia hata sijui nisemeje.Views 50k ndani ya masaa 12..  Asante Mungu na kila mmoja wenu ambayeametazama ushuhuda huu wangu. Ni heri upande wa Mungu," DJ Fatxo alisema kwenye Facebook.

Mwimbaji huyo amerejea tena kwenye muziki wiki chache tu baada ya DPP kumwondolea tuhuma za mauaji kufuatia kifo cha kijana wa miaka 23, marehemu Jeff Mwathi aliyefariki nyumbani kwake mapema mwaka huu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji alieleza ni kwa nini hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mbunifu huyo wa mapambo ya ndani.

Katika barua kwa Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) iliyotiwa saini na mkurugenzi msaidizi wa mashtaka ya umma Gikui Gichuhi, DPP aliweka wazi kwamba hakuna ambaye alipataikana na hatia.

Akizungumza wakati wa mahojiano na Massawe Japanni katikati mwa mwezi jana, DJ Fatxo alisema kwamba marehemu alikuwa rafiki yake na kubainisha kuwa hakuwa na sababu yoyote ya kumdhuru.

"Jeff alikuwa rafiki yangu. Sioni sababu yangu kumuua," alisema.

Hata hivyo, aliweka wazi kwamba urafiki wao haukuwa wa karibu bali ulikuwa wa kikazi.

Hatukuwa na urafiki wa karibu. Ilikuwa tukipatana tu wakati nanunua viatu," alisema.