Mchekeshaji maarufu wa Kenya Eric Omondi ametangaza kuwa anamtafuta mama wa mtoto aliyenaswa kwenye picha ya selfie na kaka yake, marehemu Fred Omondi.
Katika chapisho la Jumatatu, mchekeshaji huyo wa zamani wa kipindi cha churchill alionyesha screenshot ya chapisho la zamani la Fred akiwa amemshika msichana huyo mrembo.
Marehemu Fred, katika posti hiyo, alimtambulisha msichana huyo mdogo ambaye alikuwa amemshika kama "Penzi wa moyo.
Picha hiyo ilinasa matukio mazuri kati ya wawili hao huku wakitumia muda pamoja ndani ya nyumba. Fred hata hivyo hakubainisha iwapo msichana huyo ni binti yake, lakini alidokeza hivyo.
Mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi sasa ametoa wito kwa wanamitandao kumsaidia kumpata mama wa mtoto huyo.
“Natafuta mama ya huyu mtoto,” Eric aliandika.
Eric baadaye alifuta chapisho hilo kwa sababu zisizojulikana.
Marehemu Fred Omondi ambaye alipoteza maisha katika ajali mbaya iliyotokea kwenye Barabara ya Kangundo mnamo Juni 15 alikuwa ameficha maisha yake ya mahusiano na sio mara nyingi ambapo alizungumza kuhusu wapenzi wake au watoto wake.
Wakati wa misa ya kumbukumbu ya marehemu kwa ajili ya maandalizi ya mazishi yake, kakake Eric Omondi, alifichua kuwa tayari mama wawili wamefichua kuwa wana watoto wa Fred.
Pia alitangaza kwamba ikiwa kuna mtu mwingine yeyote anayedai kuwa na mtoto na marehemu kaka yake - basi wajitokeze kabla hajazikwa.
Omondi aliongeza kuwa yuko tayari kutunza watoto lakini tu kama wanafanana na Fred Omondi.
"Kuna watoto nyumbani wanakaa Mulamwah. Wale watu wanakuja wanasema wako na watoto wa Fred tafadhali wafanane na Fred. Wawili washafika nyumbani," Erick alisema.
Hapo awali, Fred alikuwa ametangaza hadharani kwamba alikuwa na binti wawili na kuweka wazi kuwa hana nia ya kuficha watoto wake.
Ajali iliyochukua maisha ya Fred lilitokea Juni 15 asubuhi wakati pikipiki aliyokuwa amepanda iligongwa na basi, na kumsababishia majeraha mabaya.