Mwanamitindo wa Bongo Hamisa Mobetto ameweka wazi kuwa hana kinyongo chochote na msanii mwenzake Wema Sepetu.
Wawili hao ndio mastaa wa kike wa Tanzania wanaofuatiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii na kwa muda mrefu mashabiki wao wamekuwa wakiwashindanisha na hivyo kufanya ionekana kama kwamba wanazozana.
Mobetto hata hivyo amebainisha kuwa ana uhusiano mzuri na muigizaji huyo na kufichua huwa wanawasiliana mara kwa mara.
"Hatuna utofauti. Huwa tunaongea kabisa wakati mwingi," alisema.
Mbali na wote kuwa wasanii, Mobetto na Wema pia waliwahi kuwa wapenzi wa bosi wa WCB Diamond Platnumz kwa nyakati tofauti.
Mobetto pia alikanusha madai ya kushindana na muigizaji huyo kwenye wafuasi wa mitandao ya kijamii. Alisema hajishughulishi sana na mitandao hiyo na yuko pale kwa ajili ya kutengeneza pesa tu.
"Ingekuwa sitengenezi pesa, basi nisingekuwa na akaunti. Ndio maana watu wanalalalamika kwa ukurasa wangu umejaa matangazo, lakini ndio maana niko hapo. Nahitaji kutengeneza pesa hapo," alisema.
Pia aliweka wazi kwamba hajawahi kununua wafuasi wa Instagram,
Kwa sasa mwanamitindo huyo anaikaribisha bendi ya Sauti Sol kutoka Kenya ambayo iko nchini Tanzania kwa tamasha.
Inaripotiwa kuwa mzazi mwenza huyo wa Diamond pia amechaguliwa kuwa MC katika tamasha hilo la Sauti Sol.
Siku ya Ijumaa, mwanamitindo huyo alishiriki kikao na wanahabari pamoja na watunzi hao wa Midnight Train, na kuwajulisha mashabiki wao kuwa wametua Tanzania tayari kuwa na wakati mzuri nao.
Sauti Sol walitua Tanzania wakiandamana na wasanii wa Sol Generation Bensoul na Nviiri the Storyteller.
“Asante Sana, Tanzania, Kwa Kuonyesha upendo daima kwa Sauti Sol na Kenya kwa Ujumla. Hii ni moja ya sehemu tunazopenda zaidi ulimwenguni kutumbuiza kwa sababu watu wa Dar es Sallam wanaelewa muziki ambao tumealikwa kucheza. Tunawaahidi shoo nzuri," Bien alisema kabla ya shoo hiyo.