Harmonize afunguka kuhusu kukamatwa kwake Zanzibar

Konde Boy alithibitisha alitiwa mbaroni kwa kusababisha usumbufu wakati wa kipindi kitakatifu.

Muhtasari

•Katika taarifa yake, mwimbaji huyo alifichua ataachia kibao hicho Ijumaa na kujigamba kuwa ni cha aina yake kuwahi kufanywa.

•Alitoa shukrani kwa Baraza la Sanaa la Zanzibar kwa kufikia makubaliano naye ambapo alitozwa faini na kuachiliwa huru.

Image: HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amefichua kuwa ametayarisha kibao maalum kwa kisiwa cha Zanzibar, nchini Tanzania.

Katika taarifa yake ya Jumatano jioni, mwimbaji huyo alifichua ataachia kibao hicho Ijumaa na kujigamba kuwa ni cha aina yake kuwahi kufanywa.

"Tangu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanza hata kabla ukimpata msanii aliyeimba wimbo unaoitwa Zanzibar noo nikupatie m5 kama zawadi!! Awe ametokea bara ama visiwani!!Licha ya umaarufu wake wote duniani ukijumlisha na kuwa inapokea mamilioni ya watalii kutoka mataifa mbalimbali Africa na kote duniani, huu ndio unaenda kuwa wimbo wao wa Zanzibar," Harmonize alisema kwenye Instastori zake.

Bosi huyo wa Kondegang alidokeza kuwa anatarajia wimbo kupendwa sana hasa visiwani Zanzibar na utachezwa vilabuni vyote.

Wakati huohuo, alifunguka kuhusu kipindi alipokamatwa katika kisiwa hicho kizuri wakati wa msimu wa Ramadhan. Alithibitisha kwamba alitiwa mbaroni kwa kusababisha usumbufu wakati wa kipindi kitakatifu.

"Hata mimi nilikuwa nafunga. Makelele na ibada haviendani kabisa. Ukichanganya na mihangaiko ya hapa na pale jua linapiga tunastahili kabisa kusimamishwa," alisema.

Staa huyo alitoa shukrani za dhati kwa Baraza la Sanaa la Zanzibar kwa kufikia makubaliano naye ambapo alitozwa faini na kuachiliwa huru.

Hata hivyo alidokeza kuwa alifanya wimbo huo kwa ajili ya nchi yake ya Tanzania na wala si kwa manufaa yake binafsi.

"Najua kupitia wimbo huu Zanzibar haitonisahau milele. Hata nikisahaulika mimi hii sauti itabaki vichwani mwa Watanzania wote na yeyote atoke kujanya Zanzibar au hata ukiiwaza Zanzibar,"  Harmonize alisema.

Konde Boy aliwataka mashabiki wake kusubiri kibao hicho siku ya Ijumaa,Mei 12, ambapo atakiachia.