Staa wa Bongofleva, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amekiri kukumbwa na msongo wa mawazo na kugeukia ulevini baada ya kugura lebo ya Wasafi.
Katika taarifa yake Jumatano jioni, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alikiri kuwa alizama katika mawazo baada ya kuchukua hatua hiyo kubwa miaka minne iliyopita.
“Jameni, ulevi ulininenepesha kipindi nina stress kutoka kwenye label. Ndio kitu pekee kilinipa mawazo,” Harmonize aliandika kwenye Instastories yake.
Konde Boy aliondoka kwenye lebo ya Diamond Platnumz, WCB mwaka 2019 na kwenda kuanzisha lebo yake ya muziki, Konde Music Worldwide.
Amesema amefurahishwa na upendo na sapoti ambayo amepokea kutoka kwa mashabiki wake katika miaka minne iliyopita baada ya kuwa msanii wa kujitegemea.
“Mlipo nipokea na kusimama na mimi mpaka leo, sasa mimi ni tajiri kijana sio msanii tena so ukiskia nimekunywa champagne ili tu kusiaga chakula, tajiri halewi,” alisema.
Harmonize alianza kupata umaarufu baada ya kukutana na Diamond Platnumz na kusainiwa katika WCB Wasafi mwaka 2015. Uhusiano kati ya mastaa hao wawili wa bongo fleva hata hivyo uliharibika mwaka wa 2019 ambapo Harmonize allichukua hatua ya kuondoka katika lebo hiyo na kuwa msanii huru.
Mapema mwaka huu, bosi huyo wa Konde Music Worwide aliripotiwa kupiga hatua ya kutafuta huduma za mawakili kumsaidia kuishtaki lebo ya WCB inayomilikiwa na Diamond kwa madai ya kunufaika na jasho lake.
Konde Boy alisema WCB imeshirikiana na wasambazaji wa muziki, Mziiki, kuchukua fedha zinazotokana na muziki wake akidai zilikuwa zinaenda kwenye akaunti ya lebo hiyo badala ya yake licha ya mkataba wake kusitishwa.
“Wasafi na Mziiki wameshirikiana kunichafua ila sijawakosea. Imekuwa kibarua kubwa kupata kile ambacho ni changu kutoka kwao ili niweze kulisha familia yangu kama wanavyofanya na familia zao," alisema mwezi Machi.
"Kwa nini waninyime kupata haki yangu ya Haki Miliki (IP) huku wakiendelea kukusanya pesa kutoka kwa IPs zangu kwa niaba yangu,” alihoji.
Wakati huo, wimbaji huyo wa kibao 'Single Again' alisema anakamilisha mipango na mawakili wake ili kupeleka kesi hiyo mahakamani hivi karibuni.
Pia alitoa wito kwa Waziri Msaidizi mpya wa Utamaduni na Sanaa, rapa Mwana FA, kumsaidia kutatua mzozo huo.
"Ninamtegemea atanisaidia kwa sababu nimeshindwa kukusanya mirabaha yangu ya muziki kwa miaka mitatu,” alisema.