Hisia mseto baada ya aliyedukua akaunti ya Kabarak University kutishia kuchapisha video chafu

Kijana huyo ameendelea kuwaburudisha wanamitandao kwa memes, video za Tiktok na baadhi ya matukio ambayo huenda alinasa.

Muhtasari

•Mwanafunzi wa IT wa Indonesia alichukua udhibiti wa ukurasa wa Kabarak University na amekuwa akipakia machapisho yake yakiwemo picha na video.

•Siku ya Jumatatu hata hivyo aliwashangaza wengi baada ya kudokeza mpango wa kuchapisha video chafu kwenye ukurasa huo.

Image: SCREENSHOT

Kijana ambaye alidukua ukurasa rasmi wa Facebook wa Chuo Kikuu cha Kabarak ameendelea kusababisha usumbufu kwenye mtandao.

Wiki iliyopita, mwanafunzi wa IT wa Indonesia alichukua udhibiti wa ukurasa uliothibitishwa wa Kabarak University wenye wafuasi zaidi ya elfu arobaini na amekuwa akipakia machapisho yake yakiwemo picha na video.

Hapo awali, alikuwa akichapisha kwa lugha ya kigeni hadi Jumamosi alipoanza kuwahutubia Wakenya kwa lugha wanayoelewa, Kiingereza, baada ya kugundua kuwa walikuwa wakifuatilia matendo yake kwa karibu.

"Habari zenu, hapa naomba tu nifafanue kuhusu akaunti hii iliyodukuliwa, kusema kweli nilikuwa najiburudisha tu msichukulie kwa uzito machapisho ninayochapisha, kwa mara nyingine tena samahani," aliandika Jumamosi.

Mwanafunzi huyo wa shule ya Upili aliweka wazi kuwa hana mpango wa kurejesha akaunti hiyo na kutoa changamoto kwa taasisi hiyo yenye makazi yake Baringo kujaribu kuichukua tena kutoka kwake. Hata hivyo, alikuwa mkarimu zaidi kupea taasisi hiyo chaguo jingine la kumlipa Ksh 68,000 ili kuwarejeshea akaunti.

"Pia nina chaguo lingine, nipeeni tu 500$ (68,000) na nitarudisha ukurasa huu, ofa ni nafuu kwa chuo kikuu kikubwa," alisema.

Siku kadhaa baada ya kuchukua udhibiti wa ukurasa huo, mdukuzi ameendelea kuwaburudisha watumiaji wa Facebook kwa machapisho ya kusisimua, memes, video za Tiktok na baadhi ya matukio ambayo huenda alinasa.

Siku ya Jumatatu hata hivyo aliwashangaza wengi baada ya kudokeza mpango wa kuchapisha video chafu kwenye ukurasa huo.

"Je, ikiwa tutachapisha video ya ngono?" aliwauliza wanaofuatilia ukurasa huo.

Mamia ya watumiaji wa mtandao walipiga kambi kwenye chapisho hilo wakitoa hisia mseto kuhusu swali tata lililoulizwa.

Haya maoni ya baadhi ya wanamitandao;

Sakshii Chunni: Kuna suala lolote? Natumai itawaunganisha Wakenya.

Andrew Karanei: Hiyo inaweza kuwa kitu kizuri.

Ezekiel Manon: Hiyo ndiyo Wakenya wanataka. Hiyo ndiyo hutuunganisha.

Princess Graciey: Tuko na kazi zetu za kuangazia.

Esther Caleche: Unachopigana nacho hukujui oyah! Kitakuramba.

Siku ya Ijumaa, Chuo Kikuu cha Kabarak kilitoa taarifa kuthibitisha udukuzi wa akaunti yao ya mtandao wa  Facebook.

"Tunataka kuwahakikishia washikadau wote na umma kwa ujumla kwamba tunachukua hatua zote zinazohitajika kurejesha udhibiti wa ukurasa wetu wa Facebook na kuzuia ufikiaji wowote ambao haujaidhinishwa," shule hiyo alisema katika taarifa iliyotiwa saini na Makamu Mkuu wa Chuo, Henry .K. Kiplangat.

Taasisi hiyo ilikiri kuwa udukuzi huo ulisababisha fujo ikibainisha kuwa watazuia hilo kutokea katika siku zijazo.