"Kila siku nakupenda tofauti, asante kwa kunichagua" Diana Marua amsherehekea mumewe Bahati

Diana amesema Bahati ameyafanya maisha yake kuwa bora licha ya changamoto.

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diana amembwagia mumewe sifa kemkem na kumshukuru kwa mahaba anayompa.

•Pia alidokeza kuhusu mpango wa 'siku kubwa' ambayo wengi wamekuwa wakikisia kuwa siku yao kufunga pingu za maisha.

Bahati na Diana Marua
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwanavlogu na rapa mashuhuri  Diana Marua amesifia mahusiano yake na mwanamuziki Kelvin Kioko almaarufu Bahati.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diana amembwagia mumewe sifa kemkem na kumshukuru kwa mahaba anayompa.

Mama huyo wa watoto watatu ameweka wazi kuwa Bahati ameyafanya maisha yake kuwa bora licha ya changamoto walizokumbana nazo.

"Umefanya maisha yangu kuwa mazuri kwa kila njia. Tumekuwa na heka heka zetu. Msingi wa upendo wetu umejengwa kupitia changamoto ngumu ambazo tumeshinda kwa miaka mingi," alisema Diana.

Aliambatanisha ujumbe huo mtamu na video inayomuonyesha akifurahia muda na mumewe ndani ya nyumba yao. Katika video hiyo, wapenzi hao wawili wanaonekana wakicheza densi huku wimbo mpya wa Bahati 'Abebo' ukicheza

Diana aliendelea kumhakikishia mumewe kuhusu mapenzi yake tele kwake huku akibainisha kuwa huwa yananoga kadri siku zinavyosonga.

"Kila siku, ninakupenda kwa njia tofauti. #ABEBO wangu asante kwa kunichagua siku zote hata nisipokuwa na maana wakati mwingine,  bado huwa unanielewana na nitakupenda kwa hili," Diana alisema .

Pia alidokeza kuhusu mpango wa 'siku kubwa' ambayo wengi wamekuwa wakikisia kuwa siku yao kufunga pingu za maisha.

Hivi majuzi  Diana alimuomba kwa upole na unyenyekevu mumewe Bahati kumuoa rasmi kwa kufunga ndoa takatifu naye.

Diana Marua alipkuwa akitangaza wimbo 'Abebo' ambao Bahati amemshirikisha Prince Indah alimsihi mumewe amuoe kabisa ili aweze kucheza na kufurahia kibao hicho akiwa anatembea kwenye zulia la maharusi wakielekea mbele ya madhabahu kula yamini ya kuishi milele kama mwili mmoja.

“Mpenzi wangu Bahati tafadhali nioe, nataka kutembea kwa zulia la maharusi nikifurahia mandhari ya huu wimbo,aliandika.

Diana na Bahati wamekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitano na tayari wamejaliwa watoto watatu pamoja, maabinti wawili na mvulana mmoja.