Kinaya! Gidi ashangazwa na Yesu wa Tongaren kuwalilia polisi wasimtie mbaroni

"Yesu wa Tongaren ameomba polisi wasimkamate, anasema hana makosa. Yesu anaogopa polisi? Kinaya," Gidi alisema

Muhtasari

•Gidi alikiri ameshangaa kuwa Yesu huyo wa kujitangaza anawaogopa polisi ilhali yeye ni mwana wa Mungu kama anavyodai.

•Yesu wa Tongaren anatarajiwa kufika mbele kamanda wa polisi wa Bungoma  Francis Kooli Jumatano kwa ajili ya kuhojiwa.

Gidi na Bw Eliud Simiyu

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo Gidi Ogidi ameshangaa kuwa mchungaji wa Bungoma mwenye utata Eliud Simiyu Wekesa almaarufu Yesu wa Tongaren anawasihi maafisa wa polisi wasimkamate.

Siku ya Jumatano, alikiri ameshangaa kuwa Yesu huyo wa kujitangaza anawaogopa polisi ilhali yeye ni mwana wa Mungu kama anavyodai.

"Yesu wa Tongaren ameomba polisi wasimkamate, anasema hana makosa. Yesu anaogopa polisi? Kinaya," Gidi alisema kwenye Facebook.

Haya yanajiri huku mchungaji huyo mwenye makazi yake Tongaren akitarajiwa kufika mbele kamanda wa polisi wa Bungoma  Francis Kooli. Hivi majuzi, Bw Simiyu aliagizwa kufika mbele ya Kooli siku ya Jumatano ili kuhojiwa.

Kufuatia agizo hilo, mchungaji huyo alitoa ombi kwa polisi kutomtia mbaroni huku akibainisha kuwa hana makosa yoyote.

Akizungumza siku ya Jumatatu, Simiyu alisema hajafanya kosa lolote kufanya akamatwe, akiongeza kuwa anaeneza injili pekee.

“Najua hata kamanda wa polisi aliyeniita ni binadamu mwenye hekima. Ninaelewa anataka kuzungumza nami kuhusu masuala ya kanisa langu na jinsi linavyoendeshwa,” alisema.

"Labda wanasikia mambo ambayo hayapo kwa sababu nimekuwa kwa OCPD na OCS na sina shisa, ninahubiri injili tu."

Alisema akikamatwa watakuwa wanamhujumu tu kwa sababu ni wale wa upande mbaya wa sheria ndio wanaokamatwa.

Kooli alimwita kiongozi huyo wa kanisa la New Jerusalem kuhojiwa kuhusu mafundisho ya kidini yanayodaiwa kutiliwa shaka.