King Kaka amliwaza Alpha Mwana Mtule baada ya kulazwa akiwa katika hali mahututi

King Kaka alitupilia mbali madai kuwa Mwana Mtule anatafuta kiki tu kuhusu ugonjwa wake na akafichua amelazwa hospitalini.

Muhtasari

•King Kaka ametuma ujumbe wa afueni ya haraka kwa msanii mwenzake Alpha Mwana Mtule ambaye kwa sasa amelazwa hospitalini.

•Haya yanajiri siku chache tu baada ya ripoti kuibuka mitandaoni kuwa Mwana Mtule anaripotiwa kuwa hali mahututi.

amemliwaza Mwana Mtule
King Kaka amemliwaza Mwana Mtule
Image: HISANI

Rapa Kennedy Ombima aliyefahamika kwa jina King Kaka ametuma ujumbe wa afueni ya haraka kwa msanii mwenzake Alpha Mwana Mtule ambaye kwa sasa amelazwa hospitalini.

Katika chapisho la Ijumaa asubuhi, King Kaka alishiriki video ya wimbo aliofanya na mwimbaji huyo wa nyimbo za Injili anayeugua mwaka jana na kumtaka aendelee kupigania afya yake.

“Simama imara kaka. Mungu yuko nawe @mwanamtule. Maombi njiani mwako,” King Kaka aliandika chini ya video aliyoiweka kwenye Instagram.

Rapa huyo pia alikanusha madai kuwa Mwana Mtule anatafuta kiki tu kuhusu ugonjwa wake akibainisha kuwa mwimbaji huyo amelazwa hospitalini.

Alitoa ufafanuzi huo baada ya mwanamtandao mmoja kudai kuwa Mwana Mtule haumwi badala yake anatumia madai ya ugonjwa ili kupata umaarufu zaidi.

"Nilijua yote yalikuwa kiki.. Kijana lazima ablow saa hii," @officialcastrocreatives alitoa maoni chini ya video aliyochapisha King Kaka.

King Kaka alijibu, “Unamaanisha nini? Jamaa yuko hospitali, mradi huu una mwaka mmoja uliopita.”

Haya yanajiri siku chache tu baada ya ripoti kuibuka mitandaoni kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo za injili anaripotiwa kuwa mahututi.

Video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Mwana Mtule akiwa amelala kwenye kochi huku mwimbaji mwenzake B Classic akielezea hali yake mbaya.

“Wakenya wenzangu na wanamuziki, Alpha yuko katika hali mbaya na sasa hivi hawezi hata kuongea anajichafua hivyo, tunaomba msaada wa matibabu, haongei na hata hawezi kutembea," B Classic alisema kwenye video hiyo.

B Classic aliongeza kuwa walikuwa wakimpeleka hospitali na kwamba haikuwa kiki bali ni suala zito.

Hivi majuzi, Mwana Mtule alikanusha uvumi kuwa alijaribu kujiua akisema alilishwa sumu.

“Sijafa; Namshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yangu. Nililishwa sumu kwa rafiki yangu Rongai. Nitazungumza hivi karibuni na kueleza kilichotokea kwa sababu sasa bado sijisikii vizuri… bado niko hai na polisi wanachunguza washukiwa,” Alpha alisema.

"Jameni, naumia sana nasoma comments watu wakisema…ni clout chasing tafadhali acheni, Ju ata saizi hali yangu sio nzuri vile mnafikiria, Nilipewa sumu sikujaribu kujitoa uhai" Mtule alisema.

“Nimeishi na Mungu wetu mitaani miaka tisa nikikula kwa taka taka Nilikua chokora pipa, sijawai ata fikiria kujiuwa, mbona nijaribu kuijiuwa wakati kama huu mungu Ananipanga,”

“Kipaji Mungu wetu Amenipea ni kubwa kushinda clout chasing, najua adui mnanitafuta kuniua ,nyi endeleeni tu MUNGU WETU haezi sahau Huyu Boyz 😞 #MIMI," Mwana Mtule alisema.