"Lazima tukupige tu!" Mandonga 'Mtu Kazi' atuma onyo kwa Wanyonyi baada ya kutua Kenya

Mandonga alibainisha kuwa yuko nchini kwa shughuli kazi kubwa

Muhtasari

•Mandonga aliwasili Kenya  Jumatano kabla ya pambano lake dhidi ya Daniel Wanyonyi  katika ukumbi wa KICC siku ya Jumamosi.

•"Toka nianze mchezo wangu wa Boxing, sijawahi kuahidi kwamba bondia nitampiga katika raundi ya ngapi, ila lazima apigike tu," alisema

Image: INSTAGRAM// KARIM MANDONGA

Bondia mcheshi kutoka Tanzania Karim Mandonga almaarufu 'Mtu Kazi' yuko nchini Kenya.

Mandonga aliwasili Kenya siku ya Jumatano kabla ya pambano lake dhidi ya Daniel Wanyonyi linalosubiriwa kwa hamu katika ukumbi wa KICC siku ya Jumamosi.

Alifanya mahojiano na waandishi wa habari Alhamisi asubuhi ambapo alitupa maneno ya vitisho kwa mpinzani wake Wanyonyi.

"Wanyonyi lazima tukupige tu! Unataka tunakupiga, hutaki tunakupiga! Hapa hapa Kenya," aliwaambia wanahabari.

Mandonga alibainisha kuwa yuko nchini kwa shughuli kazi kubwa ambapo baadaye anaweza kuchukua muda wa kubarizi.

"Toka nianze mchezo wangu wa Boxing, sijawahi kuahidi kwamba bondia nitampiga katika raundi ya ngapi, ila lazima apigike tu," alisema.

Bondia huyo mwenye mbwembwe nyingi aliweka wazi kwamba yuko tayari kwa pambano lake dhidi ya Wanyonyi. Alimuonya mpinzani wa Kenya kuwa tayari kushindwa.

"Nimekuja na ngumi ya kigeni, ngumi iliyozaliwa Ukraine kwenye midundo ya mabomu. Ngumi inaitwa  Sugunyoo," alisema.

Mandonga aliwashukuru mashabiki wake wa Kenya na  wa Tanzania na kuwahakikishia ushindi katika pambano hilo la Jumamosi.