Lilian Nganga: Kwa nini hupaswi kupata mtoto wakati hauko tayari

Bi Nganga alimzaa mtoto wake wa kwanza mwaka jana akiwa na umri wa miaka 37.

Muhtasari

•Lilian Nganga alinukuu kuwa wazazi tu wanapokuwa tayari kwa sura hiyo mpya ya maisha, akitaja kuwa mtu anapopiga hatua hiyo haiwezi kutenduliwa.

•Lilian Nganga na Juliani walimkaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja duniani, Utheri, mnamo mwezi Julai mwaka jana.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NGANGA

Msimamizi wa miradi mashuhuri wa Kenya, Lilian Nganga amekubaliana na maoni kuwa mwanamke anapaswa kupata mtoto pale tu anapokuwa tayari kwa hatua hiyo.

Mnamo siku ya Jumatano, mama huyo wa mvulana mmoja alishiriki nukuu ya ushauri maalum kwa wanawake kuwa wazazi tu wanapokuwa tayari kwa sura hiyo mpya ya maisha, akitaja kuwa mtu anapopiga hatua hiyo haiwezi kutenduliwa.

Katika posti yake, mke huyo wa Juliani alikubaliana na ushauri huo akitaja kwamba mwanamke hawezi kuchagua kutoka kwa uzazi mara tu anapochukua hatua ya kuzaa.

"Niliona hii mahali fulani.. kama mwanamke, mzae mtoto ukiwa tayari kwa sababu ikishafanyika, ni jambo ambalo huwezi kuchagua kutoka. nakubali! nakubali! nakubali!,” Lilian Nganga aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mke huyo wa zamani wa aliyekuwa gavana wa Kaunti ya Machakos, Alfred Mutua, ambaye kwa sasa ameolewa na mwimbaji Julius Owino almaarufu Juliani alimzaa mtoto wake wa kwanza mwaka jana akiwa na umri wa miaka 37.

Lilian Nganga na mume wake Juliani walimkaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja duniani, Utheri, mnamo mwezi Julai mwaka jana, takriban mwaka mmoja tu baada ya kuyaweka wazi mahusiano yao.

Image: INSTAGRAM//LILIAN NGANGA

Mapema mwaka huu, msimamizi huyo wa miradi mwenye amefunguka kuhusu jinsi  kulea mtoto wake wa miezi kadhaa kumekuwa hadi sasa.

Akizungumzia kuhusu jinsi ulezi wa Utheri umekuwa, Lilian alibainisha kuwa imefufua baadhi ya mambo ya kitoto aliyofanya miaka ya nyuma.

"Kulea mtoto huyu kumeamsha utoto ulio ndani yangu ambao ulikuwa umesahaulika kwa muda mrefu," Bi Nganga alisema.

Mama huyo wa mvulana mmoja aliweka wazi kuwa anafurahia sana hatua ya kumlea mwanawe na mambo ambayo imemlazimu kufanya.

"Ninaipenda kwa ajili yangu.. kwa ajili yake.. kwa ajili yetu," alisema.

Wakati akimsherehekea mwanawe mnamo Septemba mwaka jana, Bi Lilian alisema mtoto huyo wake amemletea furaha kubwa kwa kufanya aitwe mama. Aidha alifichua kuwa jina la mwanawe huyo  ni 'Utheri.

"Mnamo 22.07.22 mwendo wa saa 10.11AM, Mvulana mdogo wa ajabu alinipa jina mpya Mama. Leo singesubiri jua ili kuona tabasamu yake ya ajabu huku akitimiza miezi miwili. Utheri mvulana wangu..,” alisema kupitia Instagram. 

Pia alitumia fursa hiyo kumhakikishia mwanawe kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Utheri ni jina la Kikuyu linalomaanisha 'Mwanga.'

Katika mahojiano na Citizen Digital, Lilian alifichua kuwa angependa mwanawe awe mwanga wa dunia.

"Ningependa mwanangu akiingia kwenye chumba, kinapata mwangaza mara moja," alisema.

Alisema kuwa yeye na mumewe Juliani walikuwa makini sana wakati walipomchagulia mwanao jina la 'Utheri' ili atakapokuwa mkubwa limkumbushe kuwa nuru ya ulimwengu.

Aidha alifichua kuwa watu wamembandika jina Mama Light ilhali Juliani anaitwa Baba Light.