NIKWA NI SHOKE

Khaligraph afichua alikotoa lafudhi ya Kimarekani

Wengi wanaomtambua Khaligraph wanamjua kupendelea kutumia lafudhi ya Kimarekani kwenye nyimbo zake na anapoongea

Muhtasari

•Akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japani katika stesheni ya Radio Jambo siku ya Ijumaa, Khaligraph amefichua kuwa mazoezi mengi na ziara za Marekani zimechangia pakubwa kupata lafudhi ile 

•Khaligraph alifichua kuwa safari yake ya masomo haswa katika shule ya upili haikuwa rahisi.

Khaligraph Jones
Khaligraph Jones
Image: Radio Jambo

Wanaomtambua  mwanamuziki matata wa nyimbo za kufoka, Khaligraph Jones, wanamjua  kupendelea kutumia  lafudhi ya Kimarekani kwenye nyimbo zake au anapoongea

Wengi wamejiuliza ikawaje mzaliwa wa mtaa wa Kayole, Kenya akaweza kutwaa mtindo ule wa kuongea ilhali wazaliwa wengi wa maeneo hayo wanajulikana kutumia mtindo ya Sheng.

Akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japani katika stesheni ya Radio Jambo siku ya Ijumaa, Khaligraph amefichua kuwa mazoezi mengi na ziara za Marekani zimechangia pakubwa kupata lafudhi ile .

Khaligraph alieleza kuwa ana uwezo wa kipekee wa kubadilisha lugha ya mazungumzo kulingana na mazingira alimo.

"Ni kitu nilijifunza nilipokuwa nakua. Hata sasa najaribu kadri niwezavyo kuboresha msamiati na matamshi yangu kwa sababu nataka kuongea kwa ufasaha. Watu walinicheka sana nilipojiteza.. walianza kuuliza inakuwaje wewe umetoka Kayole na  accent yako ni ya  Kizungu." Khaligraph alisema.

Aliendelea kueleza kuwa ziara zake kuenda Marekani zilimshawishi sana kuzoea lafudhi ya kule. 

"Ukienda Marekani itabidi umezoea lafudhi ya kule. Ukiongea kwa lafudhi ya huku hawataelewa itabidi umegeuza. Angalau mimi nilipokuwa nakua nilikuwa nimefanya mazoezi sikuteseka sana nikizungumza." Aliendelea kusema.

Msanii huyo pia alifichua kuwa safari yake ya masomo haswa katika shule ya upili haikuwa rahisi.

Alieleza kuwa ilimbidi kusitisha masomo kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na ukosefu wa karo ya shule. Alisema kuwa wazazi wake waling'ang'ana sana kumsomesha hadi akamaliza.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa hajawahi kuendea hati yake ya mtihani wa KCSE. Ingawa hakufichua alama ambazo alizoa, alisema kuwa ni kati ya gredi C na D+.

"Nilikuwa mwanafunzi stadi, tangu shule ya msingi nilikuwa mwanafunzi stadi. Nilipoenda shule ya upili, kufuatia kukatizwa kwa masomo mara kwa mara, nilitaka tu kupata hati. Kwa hivyo sikupata gredi A, sikupata B, C..huku chini karibu na D, kati ya C+ na D" alifichua Khaligraph.

Alisema haya huku akiwailisha kibao chake kipya kwa jina 'Nikwa ni shoke'. 

Khaligraph Alisema kuwa jina hilo lilitokana na msemo 'Kwani ni kesho' unaovuma sana nchini kwa sasa. Alipoulizwa alikotoa msemo huo alikuwa na haya ya kusema:-

"Ni stori fulani tu ya hizi mambo za mitandao. Kama nilivyosema, mimi ni mtu ambaye wengi wanajaribu kufikia na kila siku nikiamka kila mtu ako na kitu ya kusema ju yangu. Hali ikasemekana ati Khaligraph anavaa chain ghushi. Kuna video ilienea sana na mimi nikaamua kama hii ndo inavuma acha nitaitumia kutengeneza muziki."