Kushughulikia shule pamoja na umashuhuri imekuwa ngumu- Trio Mio afunguka

Muhtasari

•Trio Mio alieleza kwamba mara nyingi anapokuwa anaelekea shuleni huwa anapatana na mashabiki wake ambao humzonga bila kupenda kwake.

•Aliweka wazi kuwa amekuwa akisoma vizuri na mara zote anapokuwa darasani huwa anaangazia masomo pekee na huwa hafikirii kuhusu muziki wake.

Trio Mio
Image: Instagram

Staa wa nyimbo za kisasa TJ Kasela almaarufu kama Trio Mio amekiri kwamba haijakuwa rahisi kwake kushughulikia hali ya umashuhuri pamoja na masomo haijakuwa rahisi kwake.

Akiwa kwenye mahojiano na Daniel Ndambuki katika kipindi cha Churchill Show, Trio Mio alieleza kwamba mara nyingi anapokuwa anaelekea shuleni huwa anapatana na mashabiki wake ambao humzonga bila kupenda kwake.

Trio Mio ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 17 alifichua kuwa baadhi ya mashabiki wake mtaani ikiwemo waendesha pikipiki wamekuwa wakimshinikiza awatunuku kwa zawadi au pesa kila wanapomuona.

"Imekuwa ngumu. Mara nyingi nikielekea shuleni unaweza pata nataka kununua chakula cha kuenda kula shule alafu  unapata mbogi ingine imenifuata nyuma wakisema lazima niwatolee fomu" Trio Mio alisimulia.

Msanii huyo alisema kuwa mara nyingi huwa hawezi kukidhi matakwa yote ya mashabiki hao kwa vile hata huwa habebi pesa nyingi akienda shule.

Mio hata hivo alisisitiza kuwa usanii wake haujaathiri masomo yake. Aliweka wazi kuwa amekuwa akisoma vizuri na mara zote anapokuwa darasani huwa anaangazia masomo pekee na huwa hafikirii kuhusu muziki wake.

"Kushughulikia muziki na masomo ni rahisi. Kila wakati mistari ikija huwa naandika vizuri, lakini haijawahi kuja mwalimu akiwa darasani. Hicho ndicho kitu cha maana kunitendekea. Haijawahi kutokea eti nianze kufikiria mambo na muziki mwalimu akiwa darasani" Mio alisema.

Mama ya mwanamuziki huyo pia alithibitiha kuwa muziki wake haujaathiri sana masomo yake kwani bado amekuwa akisoma.