Trio Mio afichua jinsi pesa zake zinavyosimamiwa

Muhtasari

•Trio Mio alifichua kuwa mama yake, Sofia Irma Sakwa amekuwa akihusika pakubwa katika usimamizi wa mapato ya muziki wake.

•Alisema licha ya kuwa ana uwezo mkubwa wa kifedha, huwa hapendelei kutembea na pesa nyingi mfukoni haswa anapokuwa anaelekea shuleni.

Image: INSTAGRAM// TRIO MIO

Licha ya kuwa na umri mdogo, mwanamuziki TJ Mario Kasela almaarufu kama Trio Mio ameendelea kubobea katika ulingo wa sanaa na kuvuma kote Afrika Mashariki.

Trio Mio ambaye ana umri wa miaka 17 amekuwa akiachilia vibao vikali kimoja baada ya kingine na kualikwa kutumbuiza kwenye shoo mbalimbali.

Swali ambalo huenda wengi wamekuwa wakijiuliza ni kuhusu jinsi pesa ambazo hupatikana kutokana na muziki wake zinavyosimamiwa ikizingatiwa kuwa bado yuko katika umri wa kubaleghe.

Akiwa kwenye mahojiano na Churchill, Trio Mio alifichua kuwa mama yake, Sofia Irma Sakwa amekuwa akihusika pakubwa katika usimamizi wa mapato ya muziki wake.

"Mamangu hunipanga mara nyingi. Huwa ananipanga kuhusu masuala ya pesa, kuzisimamia. Huwa najua vile nitacheza" Trio Mio alisema.

Msanii huyo alifichua kuwa mbali na majukumu ya kawaida ya mamake kama mzazi, yeye pia ni meneja wake wa muziki.

Trio Mio alisema kuwa baba yake ambaye pia ni mwanamuzik pia huwa anamsaidia sana katika taaluma yake hasa kwa ushauri.

"Babangu huwa ananisaidia. Huwa ananirekebisha. Anajua hayo mambo sana" Alisema.

Mio alisema licha ya kuwa ana uwezo mkubwa wa kifedha, huwa hapendelei kutembea na pesa nyingi mfukoni haswa anapokuwa anaelekea shuleni.

Alifichua kuwa imekuwa ngumu kwake kushughulikia umaarufu wake pamoja na shule kwa kuwa mara nyingi huwa anakutana na mashabiki wake ambao humzonga bila kupenda kwake.