Bobi Wine na mkewe washerehekea miaka 20 ya mahusiano na ndoa

Muhtasari

• Wine na Mkewe Barbie Kyagulanyi walisherehekea miaka 20 katika mahusiano na ndoa, siku chache tu baada ya mwanasiasa huyo kusherehekea miaka 40 ya kuzaliwa.

• Wakisherehekea hatua hii muhimu, Bobi ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook akielezea jinsi alivyomkuta mara ya kwanza mkewe.

Bobi Wine
Image: Facebook

Mwanamuziki na mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine na mkewe Berbie Kyagulanyi walisherehekea miaka 20 ya mahusiano Februari 16, katika jumbe za kukosha

Wengi wa mashabiki wao walifurahishwa na ndoa ya wawili, haswa baada ya kugundua ukweli kwamba Bobi alianza mahusiano na Barbie akiwa na miaka 20, kutokana na kwamba hivi karibuni alisherehekea siku yake ya kuzaliwa na kufikisha miaka 40.

Wakisherehekea hatua hii muhimu, Bobi ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook akielezea jinsi alivyomkuta mara ya kwanza mkewe.

“Barbie Kyagulanyi, Februari, 16 mwaka 2002, katika ukumbi wa kitaifa wa Sanaa, nilikunong’onezea maneno yangu ya kwanza maskioni mwako. Nilikuambia hadithi yangu, hofu yangu na matumaini yangu na nikakuomba uniamini. Hukusema hapana, wala hukusema ndio. Ulinishika tu mkono na kunipeleka matembezini,” alikumbuka Bobi Wine

Bobi ameelezea jinsi walivyotembea Pamoja wakiwa wameshikana mikono katika barabara ya bunge jijini Kampala akimsindikiza mkewe kuchukua teksi kuelekea nyumbani.

“Tumetembea tukiwa tumeshikana mikono katika Maisha magumu, Maisha ya ghetto, mapigano ya mitaani, rabsha za vilabu vya usiku na pia kukumbana na hali za kutishia Maisha Pamoja lakini kwa hayo yote bado hujawahi kuruhusu mkono wangu utoke mkononi mwako,” Bobi alimsifia mkewe.

Bobi ameelezea kwamba Mungu pekee ndiye anayejua wanakoelekea na kusisitiza Imani kwamba ako na uhakika kule wanakoenda ni kuzuri Zaidi ya kule wametoka na bado watazidi kuwa Pamoja.

Bobi Wine amewashangaza wengi alipoeleza kwamba walikuwa wanaigiza na mkewe huyo kama rais na mkewe katika tamthilia moja kwenye ukumbi huo, bila kujua kwamba siku moja watakuwa mke na mume.

“Dr Mercy aliandika ile tamthilia na tukajukumishwa kuigiza kama rais na mkewe kumbe mtunzi hakuwa anajua alikuwa anatimiza unabii. Vile tulivyokuwa tunaigiza ukumbini, niliyapata maneno yangu barabara kutoka ndani ya moyo wangu. Yalikuwa ni mapenzi yaliyotungwa katika Sanaa na kuzaliwa jukwaani, haukuwa upendo wa kuonana kwa mara ya kwanza, bali ni upendo uliokua na unazidi kukua,” aliandika Bobi Wine

Bobi amefichua kwamba katika safari yao ya miaka 20 kwenye mahusiano, haijakuwa rahisi hata kidogo na kusema kwamba aliahidi kutochepuka na mpaka sasa anazidi kulinda ahadi hiyo