Bei ya vyakula haipo juu, ni watu hawana pesa mifukoni! - Robert Alai

Muhtasari

• Mwanablogu Robert Alai amesisitiza bei ya vyakula haipo juu ila wakenya ndio hawana pesa za kununua vyakula hivyo.

• Amewasuta Wakenya kwamba wanatupa lawana za kupanda kwa bei za vyakula kwa idara ambazo hazihusiano na suala hilo.

Robert Alai
Image: Facebook

Mwanablogu Robert Alai amewakosoa wanaoongoza maandamano mitandaoni kutaka bei ya vyakula ipunguzwe wakitumia #lowerfoodprices huku wakilaumu idara zisizohusika hata kidogo.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Twitter, Alai alisema kwamba bei ya chakula haipo juu kama baadhi ya Wakenya wanavyodai ila ni watu hawana pesa za kumudu gharama za vyakula na bidhaa mbalimbali kama mafuta ya kupika na unga.

“Bei ya vyakula haipo juu. Watu mnahitaji kuwa na pesa mifukoni. Mnatupa lawana kwa vitu tofauti ambavyo havihusiki,” aliandika Alai.

Twitter

Maoni haya ya mwanablogu Alai yanajiri siku moja tu baada ya mtangazaji mkongwe Fred Obachi pia kupinga wale wanaoeneza kampeni hizo mitandaoni na kusema kwamba bei ya vyakula ipo chini kabisa ila madalali ndio wanaopandisha bidhaa hizo zinapofika sokoni.

“Sikiliza Wakenya, bei za vyakula nchini Kenya iko katika kiwango cha chini kabisa. Ni madalali (mnaowaita mama mboga) ambao wanawafyonza watumiaji wa bidhaa hizo na si wakulima,” aliandika Machokaa.

Kampeni hizi za mitandaoni zimeonekana kuchukua mkondo wa kisiasa baadhi ya wale wanaoegemea upande wa rais Kenyatta na Handshake wakipinga suala hilo huku wale wanaoegemea mrengo wa naibu rais William Ruto wakishinikiza kampeni hizo na kusema kwamba gharama ya Maisha imepanda tangu rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kukubali kushirikiana kwa Handshake.

Wikendi iliyopita Wakenya kutoka tabaka mbalimbali waliungana mitandaoni na kuanzisha kampeni za kuishurutisha serikali kupunguza bei ya vyakula, huku wakidai kwamba kupanda kwa bei ya vyakula vya kawaida kumefanya Maisha kuwa ghali na magumu.