"Hatuzungumzi tena!" Kartelo afunguka kuhusu ugomvi wake na Chipukeezy

Muhtasari

•Kartelo alifichua kuwa uhusiano wake na Chipukeezy sio mzuri kwa sasa baada yao kutofautiana kuhusu masuala mbalimbali walipokuwa wanafanya kazi pamoja.

•Kartelo i hata hivyo alisema yuko tayari kusuluhisha mzozo wake na Chipukeezy ingawa si hivi karibuni.

Kartelo na Chipukeezy
Kartelo na Chipukeezy
Image: HISANI

Mchekeshaji Nickson Chege almaarufu kama Kartelo amekiri kuwa kuna ugomvi mkubwa kati yake na aliyekuwa mtangazaji mwenzake Chipukeezy.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Kartelo alifichua kuwa uhusiano wake na naibu mwenyekiti huyo wa NACADA sio mzuri kwa sasa baada yao kutofautiana kuhusu masuala mbalimbali walipokuwa wanafanya kazi pamoja.

Kartelo alisema ingawa hajawasiliana na mchekeshaji huyo wa Churchill Show kwa muda mrefu, bado anamheshimu sana kwa kuwa alimsaidia kuvuka daraja nyingi katika taaluma yake ya usanii.

"Hatuzungumzi tena na hatufanyi kazi pamoja, ni mambo ya watu tu. Hatuko na uhusiano mzuri. Namheshimu sana. Kwa kiwango fulani amenifanyia mambo mengi na amenivukisha daraja nyingi. Tumesaidia sana na tumejengana. Amenisaidia sana. Kutokana na heshima hiyo siwezi kuwa na ile chuki kwa roho yangu. Tukiamua kutafutana sasa tuseme ati sasa tuko tayari kukaa chini tuzungumze, tunaweza. Licha ya hayo kuna mambo yaliendelea ambayo yalifanya tusisikizane" Kartelo alisema.

Mchekeshaji huyo ambaye amekuwa akikosekana sana mitandaoni siku za hivi majuzi hata hivyo alisema yuko tayari kusuluhisha mzozo wake na Chipukeezy ingawa si hivi karibuni.

Alisema Chipukeezy amewahi kujaribu kumtafuta baada yao kukosana ila anahisi muda wao kupatana bado haujafika.

"Mimi sijamtafuta. Lakini amewahi jaribu kunitafuta. Lakini saa hii sio wakati huo" Alisema.

Wachekeshaji hao wawili waliwahi kufanya kazi pamoja katika stesheni ya Ebru TV takriban miaka mitatu iliyopita kabla yao kukosana katika hali tatanishi.