•Mulamwah alimpiga vijembe MCA wa sasa wa wadi anayolenga kuwakilisha huku akidai kuwa amekuwa madarakani kwa muda mrefu sasa na hakujakuwa na maendeleo makubwa.
•Kufikia sasa Jalang’o, MC Jessy, Profesa Hamo na Victor Naman ni miongoni mwa wachekeshaji ambao tayari wametangaza azma ya kuwania viti mbalimbali baadae mwaka huu
Huku uchaguzi mkuu wa hapa nchini ukiwa umebakisha miezi michache kufanyika, watu wengi wa tabaka mbalimbali wameendelea kujitosa uwanjani na kutangaza azma zao za kuwania viti mbalimbali.
Wasanii wengi na watu wengine maarufu ni miongoni wa makurutu wapya wa siasa huku wengi wakionekana kumezea mate viti vya ubunge na uwakilishi wadi.
Mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah ni msanii wa hivi karibuni kufichua nia yake kuwawakilisha wakazi wa wadi ya Sirende, kaunti ya Trans Nzoia.
"Mambo yakienda vizuri naweza amua pia kuenda kujaribu na kung'ang'ania kiti cha wadi ya Sirende katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu," Mulamwah alisema akiwa kwenye mahojiano na Dr. Ofweneke.
Mulamwah alimpiga vijembe MCA wa sasa wa wadi anayolenga kuwakilisha huku akidai kuwa amekuwa madarakani kwa muda mrefu sasa na hakujakuwa na maendeleo makubwa.
Alisema iwapo ataafikia kuwania kiti hicho na akinyakue atatumia fursa hiyo kutafuta suluhu za changamoto ambazo zinakabili makundi mbalimbali ya watu katika wadi yake.
"Makundi tofauti yana mahitaji tofauti. Kuna vijana, wanawake, wazee na watoto. Vijana wengi wako na elimu lakini hawajui kufanya mambo mengine kutengeneza pesa. Wengi wao wanataka kuajiriwa. Nitakaa chini nao niwafungue akili.. Kuna vijana wengi wanaocheza soka nyumbani kwetu, wanaunda ligi lakini hawaendi mahali. Kuna mambo mengi nimewawekea. Ni watu ambao watajibadilisha , sio wanasiasa wanaowania ambao watawabadilisha" Mulamwah alisema.
Iwapo Mulamwah atatekeleza mpango wake wa kujitosa siasani atakuwa anajiunga na orodha kubwa ya wachekeshaji ambao wanamezea mate viti vya kisiasa.
Kufikia sasa Jalang’o, MC Jessy, Profesa Hamo na Victor Naman ni miongoni mwa wachekeshaji ambao tayari wametangaza azma ya kuwania viti mbalimbali baadae mwaka huu.