Umaarufu ulinitenga na familia yangu - Kartelo

Muhtasari

• Mcheshi Kartelo amefunguka kuhusu jinsi maisha yake yalivyobadilika baada yake kupata umaarufu, jambo ambalo lilimfanya awe mbali na familia yake.

• Kartelo aliwashauri chipukizi kuwa na mikakati ya kuweza kustahimili jinamizi la umaarufu ambalo huwavuruga wengi na kuwaaribia maisha.

Kartelo na bintiye
Kartelo na bintiye
Image: Instagram

Mcheshi Kartelo amefunguka kuhusu jinsi maisha yake yalivyobadilika baada ya kupata umaarufu, jambo ambalo lilimfanya awe mbali na familia yake.

Kupitia mahojiano aliyofanya na mwanablogu Mungai Eve, Kartelo alikiri kwamba kipindi anapata umaarufu , hakuwa ameutarajia na hivyo basi maisha yake yalibadilika kwa kasi sana na kujikuta kwamba anajishughulisha na harakati za kutafuta hela huku akikosa kutenga muda wa kujumuika na familia yake.

Kartelo alisema kwamba kwa sasa anataka kuchukua muda mwingi na familia yake na pia kuimarisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu.

Kulingana na mcheshi huyo, umaarufu unaweza kumfanya mtu kusahau mipango yake katika maisha na kujikuta akipambana usiku na mchana kufurahisha mashabiki ambao hata hawamjui.

 Aidha amesema kwamba watu wengi maarufu hupatwa na presha kutoka kwa mashabiki kuishi maisha ya kiwango cha juu ambacho hakiwiani na pesa wanazozipata, jambo ambalo linawafanya wengi kupatwa na msongo wa mawazo.

Aliongezea kwamba anawashukuru mashabiki wake ambao wamezidi kumpa sapoti licha ya kupotea mitandaoni kwa muda sasa.

Kartelo aliwashauri chipukizi kuwa na mikakati ya kuweza kustahimili jinamizi la umaarufu ambalo huwavuruga wengi na kuwaaribia maisha.