Jacky Vike afichua mafunzo muhimu aliyopata kutoka kwa marehemu Papa Shirandula

Muhtasari

•Amekiri kuwa mwanzoni hakutaka kuchukua nafasi ambayo alikabidhiwa kucheza ila baadae ikaja kumjengea jina kubwa katika tasnia ya filamu.

•Alisema marehemu alikuwa msukumo mkubwa katika taaluma yake na alimfunza kujiamini na kuwa na ushirikiano mzuri na wenzake.

Awinja na marehemu Papa Shirandula
Awinja na marehemu Papa Shirandula
Image: HISANI

Mwigizaji wa zamani wa kipindi cha 'Papa Shirandula' Jacky Vike almaarufu kama Awinja Nyamwalo amempa sifa marehemu Charles Bukeko kwa kumfanya kuwa mwigizaji guli.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, Awinja alifichua kuwa Bukeko ndiye aliyemshinikiza kukubali kuigiza katika kipindi maarufu cha Papa Shirandula.

Mwigizaji huyo alikiri kuwa mwanzoni hakutaka kuchukua nafasi ambayo alikabidhiwa kucheza ila baadae ikaja kumjengea jina kubwa katika tasnia ya filamu.

"Sijui ningekuwa wapi kama sikukubali kuchukua nafasi hiyo, siwezi kusema. Labda singekuwa nilipo kwa sasa ama ningekuwa mzuri zaidi, sijui. Yeye ndiye alinipa fursa hii na akajenga hili jina la Awinja" Alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema alijifunza mengi kutoka kwa gwiji huyo wa uigizaji marehemu katika kipindi cha takriban mwongo mmoja ambacho walifanya kazi pamoja kabla ya kufariki kwake.

Alisema marehemu alikuwa msukumo mkubwa katika taaluma yake na alimfunza kujiamini na kuwa na ushirikiano mzuri na wenzake.

"Yeye ndiye aliyenipa motisha na kuniambia kuwa ananiamini. Aliishi kuniambia kuwa mimi ni mnoma mpaka ikakwama ndani yangu. Alikuwa na tabia ya kupea watu motisha. Pia alitufunza kuwekeza kwa kila mmoja wetu. Alipenda kuleta watu pamoja" Awinja alisema.

Awinja alikiri kuwa alipojiunga na Papa Shirandula aliwaogopa sana waigizaji wenzake hasa aliyeigiza kama mwajiri wake, Jacqueline Nyaminde. (Wilbroda)