Betty Kyallo afunguka kuhusu uhusiano wake wa sasa na aliyekuwa mumewe Dennis Okari

Ndoa ya Betty na Okari ilidumu mwaka mmoja tu

Muhtasari

•Betty alisema uhusiano wake na baba huyo wa bintiye ni mzuri na huwa wanawasiliana mara kwa mara.

•Alisema kuwa suala la uzazi wenza ni mzuri huku akiwashauri wanandoa wengine waliotengana kushirikiana vizuri kulea watoto wao hata baada ya kutengana.

Image: HISANI

Mtangazaji na mjasiriamali mashuhuri Betty Kyalo amefunguka kuhusu uhusiano wake wa sasa na baba ya mtoto wake Dennis Okari.

Watangazaji hao wawili wawili walitengana takriban miaka sita iliyopita baada ya kuwa kwenye ndoa kwa kipindi kifupi.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi majuzi, Betty alisema uhusiano wake na baba huyo wa bintiye ni mzuri na huwa wanawasiliana mara kwa mara.

Betty aliweka wazi kuwa ushirikiano wake na Okari katika malezi ya binti yao Ivanna ni mzuri na wameupatia kipaumbele.

"Huwa tunashirikiana katika malezi. Huwa tuzungumza. Mazungumzo ni muhimu. Sisi sio maadui, kusema kweli sisi ni marafiki wakubwa. Huwa tunahakikisha kuwa Ivanna amepata maisha mazuri kwa kuwa anayastahili. Yeye hakuwepo wakati maneno yetu yalitokea, hana hatia," Betty alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema kuwa suala la uzazi wenza ni mzuri huku akiwashauri wanandoa wengine waliotengana kushirikiana vizuri kulea watoto wao hata baada ya kutengana.

Betty na Okari walifunga pingu za maisha mwaka wa 2015 kisha wakatengana mwaka mmoja baadae katika hali tatanishi.