'Siwezi oa', akiri Eric Omondi

Muhtasari

• Anaposherehekea miaka 40 ya kuzaliwa, mchekeshaji Eric Omondi amesema kwamba hana mpango wa kuingia katika ndoa kwa sababu rafiki zake wanaendelea kutoroka kutoka kwa ndoa.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji Eric Omondi amesema kwamba hana mpango wa kuingia katika ndoa kwa kile alichokitolewa mfano kwamba Rafiki zake na watu wa ukoo wote wanakimbia kutoka kwa ndoa na yeye haoni sababu ya kukimbilia ndoa wakati watu wanaikimbia.

Akizungumza na Oga Obinna, Omondi alisema kwamba siku zote amekuwa na masuala mbalimbali kuhusu ndoa na hajafikia mwafaka wa kuyatatua na kuona kama ataingia katika ndoa.

“Niko na maswala kadha kuhusu ndoa, kwa sababu Rafiki zangu wote wameingia katika ndoa na kuachana. Binamu zangu wote, sio wengi wao. Wote! Wameachika katika ndoa. Sasa najiuliza, kama unaenda mjini katika duka la kununua kitu, ufike hapo upate watu wanakimbia wanatoka, utataka kuingia hapo?” aliuliza Omondi.

Mchekeshaji huyo ambaye aliulizwa swali hilo kwa nini hataki kutulia na mpenzi katika ndoa haswa kwa sababu anaelekea kusherehekea miaka 40 tangu kuzaliwa alitolea mfano huo kwa nadharia kwamba hawezi ingia katika ndoa hali ya kuwa Rafiki zake wote wanakimbia kutoka kwenye ndoa.

Omondi alitangaza kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na kufika miaka 40 tarehe 9 Machi ambayo ni Jumatano wiki ijayo katika mgahawa wa Forty 40 ulioko katika mtaa wa Westlands, Nairobi.

Matamshi haya yanakuja siku chache tu baada ya mchekeshaji huyo kusema kwamba mpenzi wake alimuacha hata baada ya kujitolea na kumfanyia mambo mengi ikiwemo kulipia picha yake kwenye bango la biashara.