Profesa Hamo afunguka kuhusu sababu za kuagiza vipimo vya DNA wakati wa mzozo wake na Jemutai

Muhtasari

•Hamo alikiri kuwa ni kweli aliagiza vipimo vya DNA vifanyike ili kubaini iwapo yeye ndiye baba mzazi wa watoto wa Jemutai.

•Mchekesheji huyo aliweka wazi kuwa hajuti hatua alizochukua wakati huo kwani ni mambo ambayo walilazimika kupitia kufuatia mzozo wao.

Image: INSTAGRAM// PROFESA HAMO

Mchekeshaji mashuhuri Herman Kago almaarufu Professor Hamo amefunguka kuhusu mzozo wake wa hapo awali na mama watoto wake wawili Stella Bunei (Jemutai).

Akiwa kwenye mahojiano na Tuko Extra, Hamo alikiri kuwa ni kweli aliagiza vipimo vya DNA vifanyike ili kubaini iwapo yeye ndiye baba mzazi wa watoto wa Jemutai.

Mchekeshaji huyo alisema huo ni utaratibu ambao alilazimika kuupitia pamoja na Jemutai katika kipindi cha ugomvi ambacho walikuwa wanapitia.

"Nilifanya vipimo vya DNA. Nadhani kwa kila mahusiano mkijipata kwa ngori kama hizo, hata wanasaikolojia wanasema hayo ni mambo ambayo lazima yafanyike. Sikujua unapopitia mambo magumu na mpenzi wako, unakabiliana na mambo mengine kama hayo. Ni hatua ambayo lazima tungepitia pamoja. Nilitaka iwe kati yangu na yeye tu lakini kwa namna fulani ikafikia vyombo vya habari na kila mtu akalizungumzia," Hamo alisema.

Kulingana na Hamo, mahusiano yote hukabiliwa na changamoto kama zile walizokumbana nazo na mchekeshaji huyo mwenzake ila haziangaziwi sana wakati wahusika ni watu wasio na umaarufu kama ule wao.

"Ilibidi tukabiliane nalo hivo tu. Ni mahali ambapo watu hujipata tu. Ata hamjui yakifanyika. Wanasaikolojia na watu ambao mnazungumza nao ndio huwasaidia kukabiliana nayo. Mnaweza kujipata mkikabiliana na mambo hayo huko mbele, Ni jambo ambalo hatukuwazia hapo awali lakini ni sehemu ya kipindi tulichokuwa tunapitia," Hamo alisema.

Mchekesheji huyo aliweka wazi kuwa hajuti hatua alizochukua wakati huo kwani ni mambo ambayo walilazimika kupitia kufuatia mzozo wao.

Hamo alisema kuwa tayari mzozo wake na Jemutai umesuluhishwa na wanalea watoto wao vizuri pamoja. Hata hivyo alifichua kuwa wao sio wanandoa.