Eric Omondi asimulia alivyotiwa mbaroni na baba yake polisi kwa kubugia Busaa

Muhtasari

•Eric Omondi alifichua kuwa baba yake aliwahi kumtia mbaroni mara tatu katika siku za ujana wake.

•Amesema kando na kukamatwa mara tatu katika utoto wake, alikamatwa tena hivi majuzi tu alipoongoza maandamano jijini Nairobi.

Image: INSTAGRAM.// ERIC OMONDI

Mchekeshaji mashuhuri Eric Omondi amefunguka kuhusu changamoto za kulelewa na baba ambaye ni afisa wa polisi.

Akiwa kwenye mazungumzo na Oga Obinna, Omondi alifichua kuwa baba yake aliwahi kumtia mbaroni mara tatu katika siku zake za utotoni.

Mchekeshaji huyo alisimulia jinsi baba yake ambaye alikuwa Inspekta wa polisi aliamuru akamatwe baada ya kupatikana katika hafla ya 'Disco Matanga.'

"Mama na baba wakiondoka tulikuwa tunahepa. Babangu hakuwahi kujua. Wakati mmoja polisi walikuja na hawangeweza kututambua. Walikuja wakaegesha lori lao kwa mlango, ukikimbia ungejipata ndani tu. Watu walipokuwa wanaingia afisa mmoja alinitambua kama mtoto wa Inspekta Omondi kisha akaniachilia. Mimi nilitoka nikaenda. Siku iliyofuata wakati babangu alienda kazini, afisa yule alichoma. Alidhani kuwa babangu angefurahi. Babangu aliuliza ni mtoto wake yupi ambaye alikuwa amekamatwa kisha afisa huyo akasema ni Eric. Walichoma wakasema kuwa waliniachilia kwa sababu nilipatikana na makosa mawili, alinipata na Busaa kwenye Disco," Eric alisema.

Eric alisema babake alituma kikosi cha maafisa kwenye hoteli ya mamake alikokuwa. Alitiwa pingu, akapelekwa kituoni na kuzuiliwa kwa usiku moja.

Mara ya pili mchekeshaji huyo alikamatwa pamoja na ndugu yake mkubwa Fred Omondi baada ya kumfanyia mvulana mwingine mzaha na kumsababishia majeraha mabaya kwenye mguu.

"Baba alipiga simu akaita polisi wengine ili tukujiwe," Alisema.

Eric alisema kando na kukamatwa mara tatu katika utoto wake, alikamatwa tena hivi majuzi tu alipoongoza maandamano jijini Nairobi.