Laana ya kizazi? Eric Omondi ataja sababu zake kususia ndoa

Muhtasari

•Eric alikiri kuwa kuna masuala ambayo yanamzuia kuchukua hatua hiyo muhimu maishani  licha ya kuwa anaelekea kuhitimu miaka 40.

•Mchekeshaji huyo aliweka wazi kuwa licha ya kujaribu mahusiano mengi hajawahi kuwa kwenye ndoa yoyote na kwa sasa anajitambua kama baba ya mtoto mmoja tu.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mcheshi Eric Omondi ameweka wazi kuwa hayuko tayari kujitosa kwenye ndoa wakati wowote ule.

Akiwa kwenye mahojiano na Oga Obinna, Eric alikiri kuwa kuna masuala ambayo yanamzuia kuchukua hatua hiyo muhimu maishani  licha ya kuwa anaelekea kuhitimu miaka 40.

Baba huyo wa mtoto mmoja anayejulikana alifichua kuwa ndoa za marafiki wake wa karibu pamoja na za wajomba wake wote zimesambaratika, jambo ambalo limemfanya ahofie kutafuta jiko pia.

"Niko na tatizo kubwa na ndoa kwa kuwa marafiki wangu wote wamepewa talaka. Wajomba wangu wote wametengana na wake zao. Huwa najiuliza,ukienda jijini kununua kitu alafu ufike kwa duka upate watu wanatoka, utaingia kweli?" Eric alisema.

Mchekeshaji huyo aliweka wazi kuwa licha ya kujaribu mahusiano mengi hajawahi kuwa kwenye ndoa yoyote na kwa sasa anajitambua kama baba ya mtoto mmoja tu.

 Alisisitiza kuwa kwa sasa uhusiano wake na mama ya mtoto wake, Jacque Maribe ni mzuri na wanashirikiana vyema katika malezi ya mwanao.

"Sijui kama niko na mtoto mwingine mahali. Kwa sasa tuko sawa na Maribe," Eric alisema.

Mchekeshaji huyo pia alipuuzilia mbali madai ya kulala na wahusika wa kipindi chake cha Wife Material huku akidai kwamba hakuwahi lala na yeyote.