Diamond adokeza jina la EP yake kwa ufupisho

Muhtasari

• Diamond Platnumz ametangaza kuachia EP yake tarehe 11 Machi, na amedokeza kwamba itaitwa FOA kwa kifupi huku akiwataka mashabiki kung'amua kirefu chake.

Diamond Platnumz
Image: Instagram

Msanii Diamond Platnumz baada ya kukaa kwa muda bila kutoa ngoma moto kama ilivyokuwa kawaida yake miaka ya nyuma, sasa amerudi tena na safari hii anarudi na EP yake ambayo ni nusu ya albamu na wapenzi wa muziki wanasema hii ndio EP ya kwanza kabisa kutoka kwa msanii huyo kwani mara nyingi amekuwa akitoa singles ambazo zimefanaya vizuri kupita maelezo.

Akitoa tangazo hilo Alhamisi jioni, Diamond alidokeza kwamba EP yake ataiachia Machi 11 na ametoa jina la ufupisho wake kuwa FOA ambapo pia amewataka wafuasi na mashabiki wake kuling’amua kwa kirefu.

Wasanii mbalimbali wamefurika na kumpongeza kwa hatua hiyo na wengi hata wameshiriki kueneza tangazo hilo chini ya alama ya reli #FOATheEP.

Baadhi ya mashabiki wamejaribu pia kung’amua jina la EP hiyo kwa urefu na ubashiri wa mashabiki wengi ni vichekesho tu kwani kia mtu amejaribu kutoa yake wake almradi herufi hizo tatu zinaonekana.

“Father of Africa” mmoja alimtania.

Hii ilipokelewa kwa vicheko vingi kutoka kwa mashabiki wake ambao wengi wamekuwa wakimuita hivo kimajazi kutokana na kwamba amekuwa katika mahusiano na wanawake Zaidi ya mmoja na kuzaa nao, wengine wakiwa kutoka nje ya nchi ya Tanzania.

Ikumbukwe aliwahi kuwa katika mahusiano na mwanamitindo Hamisa Mobetto ambapo walizaa mtoto na yeye kabla ya kuachana na akaingia katika mahusiano na mfanyibiashara kutoka Uganda, Zari Hassan ambaye walizaa watoto wawili na kuachana kisha Diamond akavuka kuingia Kenya alipomchumbia mwanamuziki Tanasha Donna ambaye pia wana mtoto na yeye.

Hulka hizi za kuwa na wanawake katika mataifa mbali mbali na kuzaa nao watoto ndio ilifanya wengi kumpa jina la majazi la ‘Father of Africa’

Je, wewe unahisi kirefu cha jina hila la ‘Extended Play’ ya Diamond inayotoka tarehe 11 mwezi Machi ni gani?